Jul 07, 2022 12:27 UTC
  • Siku ya Kiswahili Duniani yaadhimishwa

Siku ya Kiswahili Duniani imeadhimishwa leo kwa mara ya kwanza baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO kupitisha tarehe 7 Julai kila mwaka kuwa siku ya kuadhimisha lugha ya Kiswahili kimataifa.

Hatua hiyo iliifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha pekee kutoka bara la Afrika kupewa siku yake maalumu ya utambulisho na kuadhimishwa.

Kiswahili hadi sasa tayari kinatambulika kama miongoni mwa lugha rasmi kwenye Muungano wa Afrika, na kinatumika kama lugha rasmi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na Bunge la Afrika na ni moja ya lugha za Afrika zinazozungumzwa na watu wengi duniani.

Sherehe za mwaka huu zinakuja siku chache tu baada ya Baraza la Mawaziri Uganda kuidhinisha Kiswahili kama lugha rasmi ambayo pia sasa itakuwa somo la lazima katika  shule za msingi na upili nchini humo.

Katibu Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay, ametuma ujumbe kwa mnasaba wa Siku ya Kiswahili Duniani na kusema lugha hiyo ina nafasi muhimu katika kuhimiza mazungumzo baina ya watu wa mataifa mbali mbali na kwamba ni lugha yenye nguvu ya kuleta umoja.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC Dkt. Peter Mathuki

Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC Dkt. Peter Mathuki amesema wananchi wa bara zima la Afrika wajiandae kunufaika na lugha hiyo.

Aidha amesema lugha hii itasaidia pakubwa hasa kwenye ukuaji wa jumuiya na kuelewana kwa mambo tofauti.

Halikadhalika, Mathuki, amepongeza na kulishukuru shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO kuitambua na kuikubali lugha ya Kiswahili kwa umuhimu wake na kuitengea siku rasmi ya kuadhimishwa tarehe 7 mwezi wa 7.

Amekumbusha watu wote wanaozungumza lugha ya Kiswahili kuendelea kukienzi na kuhamasisha wengine wazungumze lugha hiyo.