Jul 08, 2022 02:08 UTC
  • Rais wa Somalia: Ukifika wakati mwafaka tutafanya mazungumzo na Ash-Shabaab

Rais mpya wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud amesema, kuhitimisha uasi wa utumiaji silaha unaofanywa na kundi la Ash-Shabaab unahitaji mbinu nyingine kuliko ya kijeshi na kwa hivyo utakapofika wakati mwafaka, serikali yake itafanya mazungumzo na kundi hilo lenye misimamo ya kufurutu ada.

Rais wa Somalia amesema, kundi hilo lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda, likiwa linahusika na mashambulio ya umwagaji damu katika ukanda wa Afrika Mashariki limeshahodhi na kupata uzoefu kamili wa kutekeleza hujuma za kijeshi na kwa hivyo haliwezi kutokomezwa kwa kutumia nguvu pekee. Amefafanua kwa kusema, hata kama silaha na zana zao za kijeshi zitaangamizwa, wanamgambo wa Ash-Shabaab wanao uwezo wa kujipanga upya na kurudi tena kwenye uwanja wa mapigano.

Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia

Mohamud ambaye alichaguliwa kuwa rais wa Somalia mwezi Mei mwaka huu, akiwa tayari ameshawahi kushika wadhifa huo kuanzia 2012 hadi 2017, amesisitiza kuwa, mbinu zilizotumika huko nyuma dhidi ya Ash-Shabaab hazikuwa na tija, kwa hiyo serikali yake iko tayari kwa hatua mbadala ikiwemo ya mazungumzo itakapohitajika kufanya hivyo.

Akihutubia hadhara ya wanafikra akiwa ziarani nchini Uturuki, rais wa Somalia amesema: "kwa sasa hatuko katika mazingira ya kufanya mazungumzo na Ash-Shabaab. Tutafanya hivyo katika muda mwafaka".

Wanamgambo wa Ash-Shabaab walitimuliwa katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, mwaka 2011 na kikosi cha Umoja wa Afrika, AMISOM; hata hivyo kundi hilo lingali linashikilia baadhi ya maeneo ya mashambani na lina uwezo wa kufanya hujuma na mashambulio ya mara kwa mara ya umwagaji damu yanayolenga wanajeshi na hata raia.../

Tags