Jul 11, 2022 11:09 UTC
  • Wakenya milioni 14 wanasumbulia na njaa huku mgogoro wa chakula ukishtadi

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema Kenya ni miongoni mwa nchi 63 duniani zenye idadi kubwa ya watu wanaokabiliwa na lishe duni kutokana na uhaba wa chakula.

Taasisi hizo za UN kama vile Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Shirika la Afya Duniani (WHO) zimesema Wakenya milioni 14.4 walishuhudia uhaba wa chakula katika kipindi cha kati ya mwaka 2019 na mwaka jana 2021.

Ripoti ya taasisi hizo imeeleza kuwa, kufikia mwaka 2020, Wakenya milioni 43.6, katika taifa lenye jamii ya watu milioni 53, walishindwa kumudu lishe bora inayozingatia viwango vya afya na virutubisho.

Imesema watoto zaidi ya milioni moja wenye umri wa chini ya miaka mitano wana utapiamlo mkubwa, hususan katika maeneo ya kaskazini na kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Watoto ndio wahanga wakubwa wa mgogoro wa chakula duniani

Kwa mujibu wa ripoti ya taasisi hizo za UN, watu milioni 828 (karibu asilimia 10 ya jamii ya watu wote duniani) mwaka jana 2021, waliathiriwa na njaa, likiwa ni ongezeko la milioni 46 ikilinganishwa na mwaka juzi 2020, na milioni 150 mwaka 2019.

Mashirika hayo yamesema kwa ujumla watu bilioni 2.3 walishuhudia uhaba wa chakula kwa kiwango cha juu na cha wastani mwaka uliopita 2021 katika kona mbalimbali za dunia.

Tags