Jul 15, 2022 02:29 UTC
  • UN yalaani wimbi la hujuma dhidi ya raia mashariki mwa Kongo DR

Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amelaani wimbi la mashambulio yanayofanywa na wanamgambo wa Allied Democratic Forces (ADF) dhidi ya raia katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Bintou Keita amesema katika taarifa kuwa, kuna haja ya kuimarisha operesheni za kijeshi dhidi ya ADF na magenge mengine ya waasi yanayofanya hujuma za umwagaji damu katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri, kaskazini mashariki mwa nchi.

Amesema tangu wiki iliyopita, wapiganaji wa ADF wameua zaidi ya raia 20 mbali na kuteka nyara makumi ya wengine, wakiwemo watoto 30, katika maeneo ya mashariki mwa DRC.

Keita ambaye pia anaongoza Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO amesema harakati za ADF zimeongezeka kwa kuwa askari wa kikosi hicho cha UN wakishirikiana na wanajeshi wa Kongo kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa, wamekuwa wakishughulika zaidi kukabiliana na kundi la M23.

Askari wa DRC na UN wakilinda doria mkoani Ituri

Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa UN nchini DRC ameyataka makundi yote ya wanamgambo nchini humo yasichukue hatua zozote za kuchochea taharuki zaidi, na yaweke chini silaha pasi na masharti yoyote.

Kundi la waasi la ADF linalotokea kaskazini mashariki mwa Uganda limekuwa likiendesha shughuli zake katika maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa DRC tangu muongo wa 90, ambapo limeua mamia ya watu, na kupelekea malaki ya wengine kuwa wakimbizi.

Tags