Jul 15, 2022 02:30 UTC
  • Maelfu ya Waethiopia wakimbia mateso, manyanyaso Saudia

Makumi ya maelfu ya raia wa Ethiopia wamewasili Addis Ababa mji mkuu wa nchi hiyo, huku serikali ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika ikiendelea na zoezi la kuwarejesha nyumbani raia wake wakitokea Saudi Arabia.

Wizara ya Wanawake na Masuala ya Jamii ya Ethiopia imesema raia wapatao 50,337 wa nchi hiyo wakiwemo watoto 3,628 wamerejeshwa nyumbani katika kipindi cha siku 45 zilizopita.

Taarifa ya wizara hiyo imefafanua kuwa, Wahabeshi zaidi ya 50,000 waliorejeshwa nyumbani kuanzia mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, ni sehemu wahajiri 102,000 wa Ethiopia walioko Saudia, na wanaotazamiwa kurejeshwa nyumbani katika muda wa miezi saba hadi 11 ijayo.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), Waethiopia wasiopungua 750,000 wanaishi nchini Saudia na kwamba 450,000 miongoni mwao waliingia nchini humo kinyume cha sheria; hivyo watahitaji msaada ili kurejea nyumbani.

Wahajiri wa Ethiopia wanavyoishi maisha ya uchochole Saudia

Mashirika ya haki za binadamu kwa miaka kadhaa sasa yamekuwa yakikosoa na kupinga mazingira na hali mbaya inayowakabili raia wa Ethiopia waliohajiri nchini Saudi Arabia.

Maelfu ya Waethiopia husafirishwa kimagendo kila mwaka katika Peninsula ya Kiarabu kupitia Djibouti na Yemen, na hivyo kujiweka katika hatari ya ama kufungwa jela au kuuawa.

Tags