Jul 16, 2022 02:46 UTC
  • AU yatuma askari polisi wapya 160 wa Nigeria huko nchini Somalia

Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) kimepokea askari polisi 160 kutoka Nigeria, watakaikisaidia katika jitihada za kurejesha uthabiti katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Hayo yametangazwa na Mohammed Ibrahim, kamanda mkuu wa Kikosi cha 11 cha Jeshi la Polisi la Nigeria (NFPU) ambaye ameeleza kuwa, askari polisi hao wa Nigeria wanatazamiwa kupiga jeki usalama wakati huu wa kipindi cha mpito kwa vikosi hivyo vya kieneo.

Amesema, "Maafisa hawa wamepewa mafunzo ya kutosha na nidhamu. Wanatazamiwa kutekeleza majukumu waliyopewa na Umoja wa Afrika."

Haya yanajiri siku chache baada ya msafara wa Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) kugonga bomu la kutegwa ardhini kwenye viunga vya Marka, kusini magharibi mwa eneo la Lower Shabelle, ambapo askari 5 waliuawa.

Uganda pia ina askari polisi ndani ya kikosi cha AU nchini Somalia

Mwezi Aprili mwaka huu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipangua Kikosi cha Kijeshi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) na kuunda kikosi kipya cha mpito cha ATMIS. Kikosi hicho cha mpito cha AU kinatazamiwa kumaliza shughuli zake Disemba mwaka 2024.

Wanamgambo wa Al-Shabaab walitimuliwa katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, mwaka 2011 na kikosi cha Umoja wa Afrika, AMISOM; hata hivyo kundi hilo lingali linashikilia baadhi ya maeneo ya mashambani na limeendelea kufanya hujuma na mashambulio ya mara kwa mara ya umwagaji damu yanayolenga wanajeshi na hata raia.

Tags