Jul 16, 2022 07:51 UTC
  • Rached Ghannouchi
    Rached Ghannouchi

Kiongozi wa chama cha Ennahda cha Tunisia, Rached Ghannouchi, amesema kwamba Rais Kais Saied anatumia kura ya maoni juu ya katiba mpya kuimarisha udikteta, akionya kwamba hali ya Sri Lanka inaweza kujikariri nchini Tunisia.

Ghannouchi, ambaye alikuwa spika wa bunge hadi Saied alipolifuta kazi na kunyakua mamlaka yote ya nchi, amesema kuwa mazingira ya kuelekea kwenye kura ya maoni iliyopangwa kufanyika Julai 25 hayakuwa ya kidemokrasia.

Ghannouchi ambaye anasubiri kufikishwa mahakamani na serikali ya Rais Kais Saied kwa tuhuma za ugaidi na kutakatisha fedha chafu, ameongeza - katika mahojiano na Reuters - kwamba kukithiri kwa matatizo ya kiuchumi, upuuzaji wa rais Saied wa matatizo hayo na kujishughulisha na mabadiliko ya kisiasa tu, kunaweza kuitumbukiza Tunisia katika mlipuko wa kijamii sawa na ule ulioshuhudiwa siku chache zilizopita huko Sri Lanka. "Hali ya Sri Lanka inainyemelea Tunisia", amesema Rached Ghannouchi.

Ghannouchi amekuwa mhusika mkuu katika siasa za Tunisia tangu mapinduzi ya mwaka 2011 yaliyomng'oa madarakani rais wa zamani, Zine El Abidine Ben Ali, kuanzisha demokrasia na kuibua kile kilichojulikana kama Msimu wa Machipuo wa Kiarabu (Arab Spring).

Hata hivyo, kushindwa kwa mipango ya kiuchumi katika serikali zote zilizofuatana tangu mwaka 2011 kumezidisha hali ya ghasia na mvutano baina ya watu wa Tunisia ya serikali ya nchi hiyo.

Tags