Jul 17, 2022 11:11 UTC
  • Amnesty yamwandikia barua Rais wa Tanzania kupinga kesi ya mauaji inayowakabili Wamaasai 25

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limemwandikia barua Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kutaka operesheni maalumu ya kuwahamaisha watu wa jamii ya Maasai kutoka Loliondo katika mbuga ya taifa ya Serengeti, isitishwe mara moja.

Katika barua yake hiyo, shirika la msamaha duniani limemsihi rais Samia atoe maagizo ya kuachwa mara moja hatua ya kuwaondoa wamaasai kutoka sehemu hiyo hadi "wamaasai watakaporidhia bila kushurutishwa na waondoke kwa hiari yao baada ya mashauriano ya wazi na haki."

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu vilevile linataka uchunguzi huru na wa kina ufanyike kuhusu makabiliano yaliyotokea kati ya maafisa wa usalama na wamaasai tarehe 9 ya mwezi uliopita wa Juni.

Amnesty International imesema, watu 25 wanazuiliwa na polisi kwa kupinga zoezi la serikali la kuwaondoa "katika ardhi yao ambayo wameishi kwa miaka mingi na ndipo wanapaita nyumbani" na kwamba "maafisa wa polisi walitumia nguvu kuwatawanya wamaasai waliokuwa wakiandamana kwa amani kupinga hatua ya maafisa wa usalama kuwafurusha makwao."

Jamii ya Maasai

Kwa mujibu wa shirika hilo la kutetea haki za biinadamu, ripoti za mashuhuda wa tukio la Juni 9 zinasema, polisi, wanajeshi na walinzi wa mbuga waliwashambulia wamaasai kwa kutumia gesi ya kutoa machozi na risasi. Watu kadhaa waliuawa na mtu mmoja ambaye ni askari polisi alifariki.

Barua ya Amnesty kwa rais Samia inasema, waliokamatwa walifunguliwa "mashtaka ya uongo yakiwemo kumuua afisa wa polisi".

Kulingana na serikali ya Tanzania, kuna umuhimu mkubwa wa kuhifadhi mazingira dhidi ya uharibifu unaofanywa na jamii ya wamaaai ambao ni wafugaji, katika mbuga ya taifa ya Serengeti.

Msemaji wa serikali ya Tanzania Gerson Msigwa amevieleza vyombo vya habari, "inachofanya serikali ni kulinda mazingira. Ni jukumu la kila serikali kufanya hivyo." Na akaongezea kwa kusema, wanaohama huko Loliondo wanafanya hivyo kwa hiari yao na bila kushurutishwa.../  

Tags