Jul 18, 2022 11:07 UTC
  • Ummy Mwalimu
    Ummy Mwalimu

Wizara ya Afya ya Tanzania imetangaza uwepo wa mlipuko mpya wa ugonjwa wa Homa ya Mgunda unaosababisha wananchi kutoka damu puani na kuishiwa nguvu na hata kufariki dunia.

Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu amesema kuwa upimaji wa sampuli za wagonjwa waliokuwa wakiugua ugonjwa usiojulikana katika Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi umethibitisha mlipuko huo kuwa wa ugonjwa wa Leptospirosis, Field Fever, kwa lugha ya Kiswahili inajulikana kama Homa ya Mgunda.

Waziri Ummy amesema hayo leo mara baada ya kutembelea Wilaya ya Ruangwa katika Mkoa wa Lindi ambako kumezuka mlipuko wa ugonjwa huo na kuzungumza na waandishi wa habari. Amesema Homa ya Mgunda ni miongoni mwa magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na unasababishwa na bakteria aina ya Leptospira interrogans.

Ummy amesema: “Ugonjwa huu umekuwepo katika maeneo ya kitropiki ambayo ni yenye hali ya joto katika mabara ya Amerika ya Kaskazini, Amerika ya Kusini, Afrika, Asia na Australia." 

Amesema: Wanyama aina za panya, kindi, mbweha, kulungu, swala na wanyamapori wengine wameripotiwa kupata maambukizi ya vimelea hivi na kuwa chanzo cha maambukizi kwa Binadamu. Ameongeza kuwa, ugonjwa wa Homa ya Mgunda huambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa Binadamu kupitia uchafuzi wa mazingira ikiwemo vyanzo vya maji.

Ugonjwa huo huambukizwa hupitia mkojo wa wanyama kwenye vyanzo vya maji ambapo tayari dawa imepatikana sanjari na namna ya kujikinga.

Hadi sasa watu 20 wameugua ugonjwa huo wilayani Ruangwa mkoani Lindi nchini Tanzana na wengine watatu wamefariki dunia, huku wawili wakiwa kwenye uangalizi maalumu.

Tags