Jul 20, 2022 11:52 UTC
  • Tunisia:Kiongozi wa chama cha An Nahdhah aachiwa baada ya kusailiwa

Kiongozi wa chama cha Kiislamu Tunisia cha An Nahdhah ameachiwa huru na kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kuhojiwa kwa muda wa masaa tisa.

Rashid Ghanushi amehojiwa na polisi wa kupambana na ugaidi wa Tunisia ikiwa zimesalia siku kadhaa hadi kufanyika kura ya maoni kuhusu katiba. Samir Dilou Wakili wa Ghanoush na afisa wa zamani wa chama cha An Nahdhah ameeleza kuwa, polisi wa kupambana na ugaidi wamemuachia huru mteja wake baada ya kusailiwa kwa masaa kadhaa. Wafuasi wa Ghanushi walikuwa na hofu kwamba kiongozi huyo wa An Nahdhah angetiwa nguvuni baada ya kusailiwa. 

Zaidi ya gari za polisi 20 zilikuwa mbele ya makao makuu ya kituo cha kupambana na ugaidi mjini Tunis ambako makumi ya wanaharakati wa chama cha An Nahdhar walikusanyika kumuunga mkono kiongozi wao. 

Wafuasi wa Ghanushi walisikika wakitaja jina la kiongozi huyo wakati akiingia mjengoni huku wakionyesha alama ya ushindi na kupunga mabango mbalimbali yaliyokuwa yameandikwa kwa lugha za Kiingereza na Kiarabu kupinga ukandamizaji huko Tunisia.

Rashid Ghanushi mwenye umri wa miaka 81 amekuwa akichunguzwa tangu mwezi Juni mwaka huu kufuatia madai ya ufisadi na kutakatisha fedha. Madai hayo yanahusishwa na miamala ya kuhamisha fedha kutoka nje ya nchi kwenda kwa taasisi ya Namaa Tunisia yenye mfungamano na chama cha An Nahdhah. 

 

Tags