Jul 22, 2022 03:12 UTC
  • Al-Shabaab yaua watu 17 katika shambulio karibu na Ethiopia

Kundi la kigaidi la al-Shabaab la Somalia limefanya shambulio nadra karibu na nchi jirani ya Ethiopia, lililopelekea kuuawa watu wasiopungua 17, wakiwemo raia watatu.

Kamanda wa Polisi ya Ethiopia alitangaza habari hiyo jana Alkhamisi na kueleza kuwa, maafisa kadhaa wa jeshi la polisi la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika wameuawa katika hujuma hiyo.

Amebainisha kuwa, wanachama 63 wa genge hilo la kigaidi na ukufurishaji na lenye mfungamano wa na mtandao wa wal-Qaeda wameangamizwa pia kwenye shambulio hilo.

Inaarifiwa kuwa, wanachama wa al-Shabaab siku ya Jumatano walishambulia vijiji viwili vya Yeed na Aato, vilivyoko katika eneo la Bokool, mpakani mwa Somalia na Ethiopia na kufanya ukatili huo.

Ramani inayoonesha mpaka wa Ethiopia na Somalia

Habari zaidi zinasema kuwa, kundi hilo la kigaidi lenye makao yake nchini Somalia lilishambulia vijiji hivyo karibu na mpaka wa Ethiopia, siku chache baada ya kamanda wake wa ngazi ya juu kuuawa ndani ya ardhi ya Uhabeshi.

Wanamgambo wa genge hilo walitimuliwa katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, mwaka 2011 na kikosi cha Umoja wa Afrika, AMISOM; hata hivyo kundi hilo lingali linashikilia baadhi ya maeneo ya mashambani na lina uwezo wa kufanya hujuma na mashambulio ya mara kwa mara ya umwagaji damu yanayolenga wanajeshi na hata raia ndani na nje ya nchi.

Tags