Jul 22, 2022 11:57 UTC
  • Watu kadhaa wauawa katika mapigano kati ya vikosi vya usalama vya Libya mjini Tripoli

Mapigano makali yaliyozuka kati ya makundi yanayohasimiana katika mji mkuu wa Libya, Tripoli, yamesababisha vifo vya watu kadhaa huku kukiwa na wasiwasi kwamba huenda mzozo wa kisiasa ukazusha upya nchini humo.

Mapigano hayo yametokea mapema leo Ijumaa katika wilaya ya kati karibu na hoteli ya Radisson Blu, eneo ambalo ni makao ya mashirika kadhaa ya serikali na jumuiya za kimataifa na vileviile makazi ya wanadiplomasia.

Mapigano hayo ya silaha nyepesi na za kati yalipanuka zaidi katika maeneo ya makazi ya raia mjini Tripoli, kama vile Al-Fernaj na Zawiyat al-Dahmani, na kusababisha hali ya hofu miongoni mwa wakazi wa maeneo hayo.

Ripoti zinasema watu wasiopungua 5 wameuawa katika mapigano hayo. Osama Ali, msemaji wa Idara ya Huduma za Dharura ya Libya, amesema kwamba takwimu za watu waliouawa katika machafuko hayo ya Tripoli zinaweza kuongezeka kutokana na ripoti zinazotolewa na hospitali za eneo hilo.

Baraza la Uongozi wa Libya limetoa wito kwa pande zote katika mzozo huo kusitisha mapigano na kurejea katika makao yao makuu.

Baraza hilo pia limemtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwendesha Mashtaka wa Kijeshi kuanzisha uchunguzi wa kina kuhusu sababu za mapigano hayo, na limewataka Waziri wa Ulinzi na Mambo ya Ndani wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuchukua hatua zinazohitajika ili kurejesha usalama katika mji mkuu wa Libya.

Libya imeathiriwa na machafuko na uksoefu wa amani tangu kupinduliwa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi, mwaka 2011 kwa uingliaji wa nchi ajinabi. 

Tags