Jul 23, 2022 11:23 UTC
  • Askari 12 wa Sudan Kusini wauawa katika jimbo lenye utajiri wa mafuta

Wanajeshi wasiopungua 12 wa Sudan Kusini wameuawa huku wengine 13 wakijeruhiwa katika shambulio la waasi kaskazini mwa nchi.

Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Sudan Kusini, Lul Ruai Koang amesema askari hao wa serikali waliuawa jana Ijumaa baada ya waasi waitifaki wa kiongozi wa upinzani Stephen Buay, ambaye pia ni kamanda wa Harakati ya Watu wa Sudan Kusini SSPA, kushambulia makao makuu ya kaunti ya Mayom jimboni Unity, kaskazini mwa nchi. 

Koang amesema Kamishna wa Kaunti ya Mayom, James Chuol Gatluak, baadhi ya jamaa zake na walinzi wake wameuawa katika shambulio hilo.

Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Sudan Kusini amesema vyombo vya usalama vimeanzisha uchunguzi ili kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika wa jinai hiyo.

Bomba la kusafirisha mafuta katika jimbo la Unity lenye utajiri wa mafuta

Genge hilo la waasi limetangaza kuhusika na shambulio hilo, likidai kuwa ni la ulipizaji kisasi kwa kuwa wanajeshi wa serikali siku ya Alkhamisi waliwashambulia na kuua askari mmoja wa kundi hilo.

Sudan Kusini imekuwa katika hali ya mchafukoge tokea Disemba mwaka 2013 baada ya Rais Salva Kiir kuzozona na aliyekuwa makamu wake, Riek Machar, ambapo makumi ya maelfu ya watu wameuawa, huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.

 

Tags