Jul 24, 2022 07:24 UTC
  • Watunisia waandamana tena kupinga rasimu ya katiba iliyopendekezwa na Rais

Kwa mara nyingine tena, wananchi wa Tunisia wamemimika katika mitaa na barabara za nchi hiyo kushiriki maandamano ya kupinga rasimu ya katiba iliyopendekezwa na Rais wao, Kais Saied.

Muungano wa Uokovu wa Taifa unaojumuisha makundi na vyama vya upinzani nchini humo ndio ulioandaa maandamano ya jana katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tunis, siku mbili kabla ya kufanyika kura ya maoni ya kuamua hatima ya katiba hiyo.

Waandamanaji hao wanasisitiza kuwa, rasimu hiyo ya katiba ina vipengee ambavyo vinaweza kufungua ukurasa wa kuundwa utawala wa kidikteta nchini Tunisia.

Wanasema mchakato mzima wa kuibadilisha katiba ya nchi hiyo mbali na kufanyika kinyume cha sheria, lakini pia unakiuka misingi ya demokrasia.

Rais Kais Saeid wa Tunisia

Wananchi wa Tunisia wanatarajiwa kushiriki kura ya maoni kuhusu katiba mpya Jumatatu ya kesho Julai 25. Kwa mujibu wa rasimu iliyopendekezwa na Rais Saeid kwa ajili ya katiba mpya, kiongozi huyo ataruhusiwa kuwasilisha miswada ya sheria na kuwa na mamlaka makubwa ya kupendekeza mikataba mbalimbali na kuandaa bajeti za serikali.  

Mwaka jana, Rais huyo wa Tunisia aliifuta kazi serikali na kutwaa madaraka ya utendaji ya nchi na hivyo kuasisi utawala wa mtu mmoja.

 

Tags