Jul 25, 2022 02:28 UTC
  • Kura ya maoni ya katiba ya Tunisia katika kivuli cha maandamano ya wananchi

Wakati Tunisia ikiitisha zoezi la kura ya maoni kuhusu rasimu ya katiba mpya, maandamano ya wananchi yanayoendelea nchini humo yamegeuka na kuwa ghasia na machafuko baada ya jeshi kuingilia kati.

Katika siku chache zilizopita, mtaa maarufu wa "Al-Habib Bourguiba" katika mji mkuu wa Tunisia ulishuhudia maandamano makubwa ya kupinga kura ya maoni kuhusu rasimu ya katiba mpya ya nchi hiyo, ambapo polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji.

Rais wa Jamhuri ya Tunisia, Kais Saied, pia amewashutumu waandamanaji kuwa wanavuruga zoezi la kura ya maoni kuhusu rasimu ya katiba na ametishia kukabiliana nao. Saied amesema: "Serikali itawashughulikia vikali wale wote wanaoizuia kutekeleza wajibu wake katika kuandaa kura hii ya maoni." 

Kais Saied

Kura ya maoni kuhusu katiba mpya ya Tunisia ilipangwa kufanyika leo Jumatatu ndani ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo imetangaza kuwa zaidi ya wapiga kura milioni 9 na laki tatu wamejiandikisha kushiriki kwenye zezi hilo. 

Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, Rais wa Jamhuri ya Tunisia alichukua hatua kadhaa ambazo zimezidisha malalamiko ya kijamii na kisiasa. Mbali na kulifutilia mbali Bunge la nchi hiyo, Kais Saied pia amewapokonya wabunge kinga ya kutofikishwa mahakamani, kufuwafuta kazi wajumbe wa Tume ya Kusimamia Katiba na kuandika rasimu ya katiba mpya bila ya kuvishirikisha vyama na makundi mengine ya kisiasa. Hali hii imezidisha mivutano na malumbano ya kisiasa nchini Tunisia hasahasa suala la kuitishwa kura ya maoni ya rasimu ya katiba mpya ambalo limekabiliwa na upinzani wa vyama, makundi na asasi nyingi za kiraia na kijamii. Wapinzani wa zoezi hilo wanasema ni kinyume cha sheria za nchi. Vilevile wanasena katiba hiyo mpya itasitisha mwenendo wa demokrasia nchini Tunisia. 

Maandamano ya Watunisia dhidi ya Kais Saied

Wakosoaji wanasema rasimu ya katiba mpya inapunguza na kuhafifisha nafasi ya Bunge na taasisi nyingizi za usimamizi wa masuala ya umma, na kwamba Rais wa nchi amepewa mamlaka makubwa sana. Wakosoaji wa Kais Saied wanasema, kufanyika kwa kura ya maoni ya marekebisho ya katiba ni sehemu ya mwisho katika mfululizo wa hatua zilizochukuliwa na kiongozi huyo ili kuimarisha nafasi na mamlaka yake. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, wapinzani wa kura hiyo ya maoni ya mabadiliko ya katiba wanaviona vitendo vya Saied kama aina fulani ya mapinduzi baridi, na wana wasiwasi juu ya kurejea utawala wa kidikteta katika nchi hiyo na kuangamiza juhudi za wananchi na vyama vya siasa za kuimarisha demokrasia na kuitishwa uchaguzi huru nchini Tunisia, baada ya mapinduzi ya mwaka 2011. Kwa msingi huo katika maandamano yao ya siku kadhaa sasa, Watunisia wamekuwa wakikariri wito wa kufutiliwa mbali zoezi hilo la kura ya maoni na kuondoka madarakani utawala wa kidikteta wa Kais Saied.

Licha ya maandamano hayo yote, kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba imefanyika nje ya Tunisia, na inatazamiwa kufanyika ndani hii leo Jumatatu. Imetabiriwa kuwa ushiriki wa wananchi katika zoezi hilo utakuwa mdogo sana baada ya vyama vya siasa kutoa wito wa kususiwa kura hiyo.

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tunisia cha harakati ya Ennahda, Rached Ghannouchi, amesema: "Kura ya maoni ya katiba mpya ina lengo la kuwahadaa wananchi, na watu wenye busara na akili hawatashiriki katika kura hiyo."

Rached Ghannouchi

Kwa vyovyote vile, mzozo wa kisiasa nchini Tunisia umepanuka zaidi huku matatizo ya kiuchumi yakiendea kuchochea moto wa malalamiko  ya kijamii.

Inaonekana kuwa kwa sasa Tunisia inahitaji zaidi maafikiano ya kiuchumi na kijamii katika mazingira tulivu ya kisiasa ili kujiondoa katika mkondo wa kuelekea kwenye kufilisika, badala ya zoezi linalofanyika leo la kura ya maoni ya rasimu ya katiba mpya.

Tags