Jul 25, 2022 07:53 UTC
  • Kura ya maoni ya katiba mpya yafanyika nchini Tunisia

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa kura ya maoni ya katiba mpya ya Tunisia inafanyika leo nchini humo.

Zoezi la upigaji kura ya maoni ya katiba mpya ya Tunisia iliyopendekezwa na rais Kais Saeid limeanza mapema leo nchini humo.

Upigaji kura huo unafanyika wakati mnamo siku za karibuni, Watunisia wengi wamepinga kura hiyo ya maoni ya katiba mpya wakisema si halali kisheria, huku vyama na mirengo mingi ya kisiasa ikitangaza kususia zoezi hilo.

Kiongozi wa chama Kiislamu cha An-Nahdhah Rashid al Ghanoushi amesema kushiriki katika kura ya maoni ya katiba mpya ni kuwahadaa wananchi na ni mchezo uliopangwa ambao watu wenye akili timamu hawawezi kujihusisha nao.

Rais Kais Saeid (kulia) akizindua rasimu ya katiba mpya

Ghanoushi amebainisha kuwa Tunisia iko kwenye hali mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa na kwamba kinachofanyika leo Julai 25 kinalipokonya taifa hilo kila lilichokuwa limepata katika uhuru na demokrasia.

Katika muda wa chini ya mwezi mmoja nyuma, Rais Kais Saeid alitangaza rasimu ya katiba mpya, ambayo itamwongezea rais madaraka aliyonayo na kupunguza mamlaka ya bunge na idara ya mahakama huku taasisi za usimamizi wa mamlaka ya rais nazo pia zikifutwa.

Akthari ya vyama muhimu vya siasa na vyenye ushawishi nchini Tunisia vimeisusia kura ya maoni ya katiba inayofanyika leo vikisisitiza kuwa katiba mpya itakayopitishwa itampatia madaraka makubwa rais na kuandaa mazingira ya kurejeshwa udikteta katika nchi hiyo.../

Tags