Jul 26, 2022 03:35 UTC
  • Waandamanaji DRC wavamia ofisi za UN, wataka kuondoka askari wa MONUSCO

Wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameshambulia makao makuu ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO katika mji wa Goma, makao makuu ya mkoa uliogubikwa na machafuko wa Kivu Kaskazini ambao unapakana na Rwanda na Uganda.

Wakazi wa mji wa Goma wamesema kuwa, ujumbe wa MONUSCO unapaswa kuondoka nchini humo haraka iwezekanavyo, kwani uwepo wake haujasaidi chochote katika kurejesha usalama na uthabiti nchini humo.

Mamia ya wakazi wa mkoa huo jana Jumatatu walifunga barabara zote muhimu za mji huo kabla ya kuandamana hadi makao makuu ya kikosi cha MONUSCO, wakitaka kuondoka askari hao wa kulinda amani, kutokana na kile wanachodai kuwa, ni uzembe katika utendaji wao wa kazi kwa zaidi ya miongo miwili tangu watumwe nchini humo.

Licha ya kukabiliwa na askari polisi wa UN kwa mabomu ya gesi ya kutoa machozi, lakini waandamanaji hao waliendelea kushambulia ofisi hizo za Umoja wa Mataifa na kuchoma moto baadhi ya majengo, huku wengine wakiiba vitu vya thamani kubwa.

Helikopta zilionekana zikiwabeba baadhi ya maafisa wa UN baada ya waandamanaji hao kuwazidi nguvu na idadi maafisa usalama katika makao makuu hayo ya MONUSCO mjini Goma.

Askari wa kikosi cha MONUSCO

Itakumbukwa kuwa, wiki iliyopita makundi ya wanawake na wanaharakati wa haki za binadamu waliandamana pia kushinikiza MONUSCO kuondoka nchini humo.

Mwezi uliopita pia, wakazi wa eneo la mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walikataa pendekezo la kupelekwa katika eneo hilo askari wa kulinda amani kutoka nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki.

Tags