Jul 26, 2022 07:07 UTC
  • Tunisia yapasisha katiba mpya licha ya wananchi wengi kususia kura ya maoni

Rasimu ya katiba iliyopendekezwa na Rais wa Tunisia, Kais Saied imepasishwa licha ya kujitokeza idadi ndogo ya watu katika zoezi la upigaji kura ya maoni lililofanyika jana Jumatatu nchini humo.

Matokeo ya muda ya Kamisheni ya Uchaguzi Tunisia yanaonesha kuwa, idadi ya watu waliojitokeza kwenye zoezi hilo ni asilimia 27.5 ya wapiga kura wote milioni 9 waliotimiza masharti ya kushiriki zoezi hilo.

Taarifa ya kamisheni hiyo imesema, rasimu ya katiba mpya ya nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika imepasishwa kwa asilimia 92.3 ya kura.

Mara baada ya kutangazwa matokeo hayo, mamia ya wafuasi wa Rais Saied walikusanyika katika barabara ya Habib Bourguiba jijini Tunis kusherehekea ushindi huo.

Akthari ya vyama muhimu vya siasa na vyenye ushawishi nchini Tunisia vimeisusia kura ya maoni ya katiba vikisisitiza kuwa katiba mpya iliyopitishwa itampatia madaraka makubwa rais na kuandaa mazingira ya kurejeshwa udikteta katika nchi hiyo. 

Maandamano ya kupinga kura ya maoni Tunisia

Katiba hiyo imepasishwa katika hali ambayo, katika siku za karibuni, Watunisia wengi wamepinga kura hiyo ya maoni ya katiba mpya wakisema si halali kisheria.

Kupasishwa kwa katiba mpya nchini Tunisia kunamaanisha kuwa, Rais Kais Saied ataruhusiwa kuwasilisha miswada ya sheria na kuwa na mamlaka makubwa ya kupendekeza mikataba mbalimbali, mbali na kuandaa bajeti za serikali.  

Tags