Jul 26, 2022 11:34 UTC
  • Waziri wa mambo ya nje wa Russia aendelea na ziara yake Afrika kwa kuitembelea Uganda

Waziri wa mambo ya nje wa Russia Sergey Lavrov amewasili nchini Uganda akiendelea na zaira yake katika nchi kadhaa za Afrika.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Russia.

Akiwa jijini Kampala, Lavrov amelakiwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Entebbe na mwenzake wa Uganda Jeje Odongo.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Russia Maria Zakharova amethibitisha kuwasili kwa Lavrov nchini Uganda akichapisha picha ya mawaziri hao wawili kwenye mtandao wa Telegram.

Sergey Lavrov anatarajiwa pia kukutana na kufanya mazungumzo na rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni. Licha ya kiongozi huyo kuwa nchini humo mamlaka nchini Uganda haijatoa taarifa zaidi kuhusu ratiba ya Lavrov kwenya taifa hilo la Afrika Mashariki.

Lavrov (kushoto) baada ya kuwasili Uganda

Rais Yoweri Museveni ambaye alizuru Russia mwaka wa 2019 ametoa wito wa kuimarishwa ushirikiano zaidi kati ya nchi yake na Russia hasa katika sekta za ulinzi, usalama pamoja na uchumi.

Alipokuwa jijini Cairo siku ya Jumapili, Waziri wa mambo ya nje wa Russia aliwahakikishia viongozi wa Misiri kwamba ombi lao la kutaka nafaka kutoka Moscow litashugulikiwa.

Halikadhalika, Lavrov amefanya ziara ya kikazi nchini Kongo-Brazzaville akitarajiwa pia kuitembelea Ethiopia.../

Tags