Jul 27, 2022 12:00 UTC
  • Waliouawa katika maandamano dhidi ya walinda amani wa UN Kongo wafikia 15

Idadi ya watu waliouawa katika maandamano ya Jumanne hii kupinga uwepo wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO) huko mashariki mwa Kongo DR imeongezeka na kufikia 15.

Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Umoja wa Mataifa na serikali ya Kinshasa imesema kuwa, askari watatu wa kulinda amani wa kikosi cha MONUSCO na waandamanaji wasiopungua 12 wameuawa katika miji miwili ya mkoa wa Kivu ya Kaskazini.  

Awali ripoti zilieleza kuwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa walifyatua gesi ya kutoa machozi na risasi za moto kwa umati wa watu waliokuwa wanaandamana kwa amani, na kuua watu kadhaa na kujeruhi wengine wengi.

Waandamanaji wakipambana na polisi katika mji wa Goma, Kongo 

Tangu Jumatatu wiki hii waandamanaji wamekuwa wakikusanyika katika miji mbalimbali mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakisema kuwa wanataka kikosi cha MONUSCO kihitimishe shughuli zake na wanajeshi wa kikosi hicho waondoke  mashariki mwa nchi hiyo. Wamesema kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa kimeshindwa kupambana na makundi yenye silaha. 

Mugisho Muhindo aliyeshiriki katika maandamano ya mji wa Goma amesema kuwa kikosi cha MONUSCO kimekuwepo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa zaidi ya miaka 20, hata hivyo kimeshindwa kurejesha amani mkoani Kivu ya Kaskazini. Amesema, unawezaje kusema kundi la waasi la M23 lina silaha zaidi kuliko MONUSCO?

Mji Butembo ambao wa tatu kwa ukubwa huko Mashariki mwa Kongo siku ya Jumanne ulikumbwa na machafuko huku huduma na shughuli mbalimbali zikizitishwa. Jumanne asubuhi mamia ya waandamanaji waliizingira na kisha kuishambulia kambi ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa huko Goma. 

Tags