Jul 27, 2022 13:15 UTC
  • Museveni: Russia imekuwa rafiki mkubwa wa Afrika kwa zaidi ya karne

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema Russia ni rafiki mkubwa wa Afrika na imekuwa ikiunga mkono harakati za kupambana na ukoloni za mataifa ya bara hilo kwa zaidi ya miaka mia moja.

Rais Museveni amesema hayo katika Ikulu ya Rais mjini Entebbe katika kikao na waandishi wa habari akiwa na Waziri wa mambo ya nje wa Russia, Sergey Lavrov na kuongeza kuwa, "Afrika itaendelea kuwa na uhusiano wa karibu na Russia."

Rais Museveni amebainisha kuwa, "Mambo yanapoibuka na watu fulani wakajaribu kuchukua msimamo dhidi ya Warusi, huwa tunawahutubu kwa kusema, watu hawa (Warusi) wamekuwa pamoja na sisi kwa zaidi ya miaka 100."

Rais wa Uganda amekosoa ubeberu wa nchi za Magharibi kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwa kusema: Tumewasamehe watu waliotukoloni...watu ambao walitufanya watumwa.

Rais Yoweri Museveni ambaye alizuru Russia mwaka wa 2019 ametoa wito wa kuimarishwa ushirikiano zaidi kati ya nchi yake na Russia hasa katika sekta za ulinzi, usalama pamoja na uchumi.

Kwa upande wake, Sergey Lavrov, Waziri wa mambo ya nje wa Russia sanjari na kuashiria ushirikiano wa karibu wa nchi yake na Uganda katika nyuga za kilimo na teknolojia ya anga za mbali, amesema, "nchi mbili hizi zimeafikiana kuunda maabara ya kusaidia kupambana na magonjwa ya kuambukiza."

Lavrov nchini Uganda

Amesema, "Tunaishukuru Uganda kwa msimamo wake kwenye masuala yanayogubika (vita vya) Ukraine, mashinikizo hayajawafanya mafariki zetu kuunga mkono vikwazo dhidi ya Russia."

Lavrov ambaye tayari amewasili Ethiopia hii leo akiendelea na zaira yake katika nchi kadhaa za Afrika baada ya kuzitembelea Misri na Jamhuri ya Congo Brazaville, amevilaumu vikwazo hivyo haramu vya Wamagharibi kwa kupanda bei za chakula katika kona zote za dunia.  

Tags