Jul 28, 2022 02:23 UTC
  • Ushiriki mdogo wa Watunisia katika kura ya maoni ya marekebisho ya katiba

Hatimaye baada ya malumbano mengi, kura ya maoni ya marekebisho ya katiba ya Tunisia ilifanyika siku chche zilizopita licha ya kususiwa na kambi ya upinzani na mashirika mengi ya kiraia.

Makadirio ya awali ya Bodi Kuu ya Uchaguzi ya Tunisia yanaonesha kuwa, kiwango cha ushiriki katika kura hiyo ya maoni ya rasimu ya katiba mpya kilikuwa takriban asilimia 27.

Kura hiyo ya maoni inatambuliwa kuwa ni hatua muhimu katika historia ya kisiasa ya Tunisia. Nchi hiyo ambayo baada ya vuguvugu la wananchi mwaka 2011, tofauti na baadhi ya nchi za Kiarabu, iliweza kuendeleza mchakato wa mpito wa kisiasa katika hali ya amani ya kiwango fulani, sasa imetumbukia katika mgogoro mkubwa wa kisiasa kwa miezi kadhaa.

Katika miezi ya hivi karibuni, Rais wa Jamhuri ya Tunisia, Kais Saied, amechukua hatua ambazo zimechochea hasira za vyama vingi na raia wa nchi hiyo. Kuvunjwa kwa bunge na kufutwa kinga ya wawakilishi, kuvunjwa kwa Baraza Kuu la Mahakama la Tunisia na pia pendekezo la kuandikwa katiba mpya ya Tunisia ni miongoni mwa hatua hizo zilizotajwa na wapinzani kuwa ni mapinduzi katika medani ya siasa, huku wanasheria wakisisitiza kuwa, ni jitihada za Kais Saied za kuhodhi madaraka ya nchi.

Maandamano ya Watunisia dhidi ya Kais Saied

Vyama na makundi mengi ya Tunisia yamesusia kura hiyo ya maoni na kuitaja kuwa ni kinyume na demokrasia. Wakosoaji wanasema, rasimu ya katiba mpya inapunguza na kuhafifisha nafasi ya Bunge na taasisi nyingine za usimamizi wa masuala ya umma, na kwamba Rais wa nchi amepewa mamlaka makubwa sana. Katiba mpya ya Tunisia inampa Rais mamlaka makubwa, ikiwa ni pamoja na kwamba, waziri mkuu na mawaziri wanateuliwa na rais na anaweza kuwafukuza kazi yeye mwenyewe bila ya kushirikisha upande mwingine wa mihimili ya dola. 

Jambo lingine ni kwamba katiba mpya ya Tunisia haikuainisha mchakato wa kushtakiwa au kusailiwa rais wa nchi. Vilevile udhibiti wa mfumo wa mahakama wa Tunisia kwa kiasi kikubwa utakuwa mikononi mwa rais.

Licha ya maandamano na upinzani huo, kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba imefanyika nchini Tunisia japo kwa ushiriki wa idadi ndogo ya wananchi, yaani asilimia 27 tu ya Watunisia. Mehdi Mabrouk, Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti na Mafunzo ya Siasa za Kiarabu nchini Tunisia, anasema: Hatuwezi kukataa kwamba mnamo Julai 25, (siku ya kura ya maoni ya rasimu ya katiba ya Tunisia) tulijiunga na nchi ambazo zimekumbwa na mapinduzi. Katika nchi yetu, kumefanyika mapinduzi dhidi ya katiba. 

Kwa hakika, kiwango cha chini cha ushiriki wa wananchi katika kura ya maoni ya marekebisho ya katiba kinaakisi upinzani wa jamii dhidi ya sera za Rais Kais Saied.

Wananchi wa Tunisia ambao pia hawaridhishwi na hali ya kiuchumi ya nchi hiyo, wanayatambua mabadiliko ya katiba kuwa ni kurudi nyuma na kupoteza malengo na matunda ya vuguvugu la wananchi la mwaka 2011.

Baada ya kura hiyo ya maoni Chama cha Wokovu wa Kitaifa cha Tunisia kilitangaza kuwa: Kutoshiriki asilimia 75 ya wapiga kura katika zoezi hilo kunaonyesha upinzani wao dhidi ya mapinduzi ya Rais kais Saied.

Kwa upande wake Kais Saied ametangaza kuwa uamuzi wa kwanza baada ya kura ya maoni ya katiba ni kuandaa rasimu ya sheria ya uchaguzi, na kwamba yanayosemwa wapinzani kuhusu kura hiyo ya maoni ni porojo na upuuzi mtupu.

Hata hivyo, wapinzani wa kura ya maoni ya katiba nchini Tunisia bado wana wasiwasi kuhusu kulimbikizwa madaraka mikononi mwa mtu mmoja, yaani rais wa nchi; suala ambalo linaweza kuwa mwanzo wa mivutano ya kisiasa na ukosefu wa utulivu katika siku zijazo. 

Tags