Jul 28, 2022 02:24 UTC
  • Miripuko ya mabomu yaua watu kadhaa kusini mwa Somalia

Kwa akali watu watano akiwemo afisa wa ngazi ya juu wa serikali wameuawa katika miripuko pacha ya mabomu iliyotokea jana Jumatano kusini mwa Somalia.

Duru za kiusalama zimearifu kuwa, Meya wa mji wa Merca, makao makuu ya eneo la Lower Shabelle, Abdullahi Ali Wafow ni miongoni mwa watu waliouawa katika mripuko wa kwanza uliolenga ofisi za serikali. Walinzi wake kadhaa wamejeruhiwa.

Habari zaidi zinasema kuwa, watu watatu wameuawa huku wengine saba wakijeruhiwa katika shambulizi la pili lililolenga soko la mifugo katika mji wa Afgooye katika mkoa huo huo wa Lower Shabelle, yapata kilomita 30 kusini mashariki mwa mji mkuu Mogadishu.

Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab lenya mfungamano na mtandao wa al-Qaeda limetangaza kuhusika na shambulio la kwanza la mjini Merca, umbali wa kilomita 90 kutoka Mogadishu.

Ramani inayoonesha eneo la Lower Shabelle

Katika hatua nyingine, makumi ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wameangamizwa katika operesheni ya vikosi vya Ethiopia karibu na mpaka wa nchi hiyo na Somalia.

Televisheni ya serikali ya Ethiopia imeripoti kuwa, magaidi hao wameuawa katika makabiliano na vikosi vya kieneo kusini mashariki mwa Ethiopia, yaliyoanza tangu Jumatatu iliyopita. 

Tags