Jul 28, 2022 11:06 UTC
  • Al-Ghannouchi: Matokeo ya kura ya maoni ya katiba ya Tunisia ni kichekesho

Mkuu wa chama chenye mielekeo ya Kiislam cha "Ennahda" nchini Tunisia aliyataja matokeo ya kura ya maoni ya katiba kuwa ni "kichekesho" na kutahadharisha kuhusu uwezekano wa kutokea migawanyiko ndani ya jamii ya Tunisia.

Rachid al-Ghannouchi ameiambia televisheni ya Al-Jazeera ya Qatar kwamba kura ya maoni ya katiba ya Tunisia, ambayo imeitishwa na kufanywa na rais wa nchi hiyo, Kais Saied, ilisusiwa na asilimia 75 ya wananchi na ilikuwa kichekesho.

Al-Ghannoushi ametahadharisha kuhusu hatari ya hotuba ya Rais wa Tunisia ambaye, kwa mujibu wake, "anataka kuzusha mgawanyiko" na kuongeza kuwa: "Taratibu zilizotumiwa kuyatarisha katiba ni batili na maudhui yake ni kuimarisha mfumo wa kidikteta ambao Tunisia ilikuwa ikiishi ndani yake kabla ya napinduzi ya Januari 2011."

Kiongozi wa harakati ya la Ennahda nchini Tunisia amesema kuwa, asilimia 75 ya watu wa Tunisia hawakuitikia wito wa Rais "Kais Saied".

Tume Huru ya Uchaguzi ya Tunisia mapema Jumatano iliidhinisha rasimu ya katiba ya nchi hiyo- ambayo ilipigiwa kura ya maoni Julai 25 - kwa matumaini ya kurejesha utulivu wa kisiasa nchini humo.

Kupasishwa kwa katiba mpya nchini Tunisia kunamaanisha kuwa, Rais Kais Saied ataruhusiwa kuwasilisha miswada ya sheria na kuwa na mamlaka makubwa ya kupendekeza mikataba mbalimbali, mbali na kuandaa bajeti za serikali.  

Katika miezi ya hivi karibuni, Rais wa Jamhuri ya Tunisia, Kais Saied, amechukua hatua ambazo zimechochea hasira za vyama vingi na raia wa nchi hiyo. Kuvunjwa kwa bunge na kufutwa kinga ya wawakilishi, kuvunjwa kwa Baraza Kuu la Mahakama la Tunisia na pia pendekezo la kuandikwa katiba mpya ya Tunisia ni miongoni mwa hatua hizo zilizotajwa na wapinzani kuwa ni mapinduzi katika medani ya siasa, huku wanasheria wakisisitiza kuwa, ni jitihada za Kais Saied za kuhodhi madaraka ya nchi.

Vyama na makundi mengi ya Tunisia yamesusia kura hiyo ya maoni na kuitaja kuwa ni kinyume na demokrasia. Wakosoaji wanasema, rasimu ya katiba mpya inapunguza na kuhafifisha nafasi ya Bunge na taasisi nyingine za usimamizi wa masuala ya umma, na kwamba Rais wa nchi amepewa mamlaka makubwa sana. 

Tags