Jul 30, 2022 03:41 UTC
  • Makumi ya magaidi wauawa katika mji mkuu wa Nigeria

Jeshi la Nigeria limetangaza habari ya kuwaangamiza makumi ya wanachama wa kundi la kigaidi lililowashambulia askari wa Brigedi ya Gadi ya Rais na kuua wanane miongoni mwao mapema mwezi huu katika eneo la Bwari, mjini Abuja.

Akiongea na waandishi wa habari mjini Abuja Alkhamisi, Meja Jenerali Benard Onyeuko, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa jeshi hilo amesema magaidi 30 wameangamizwa katika operesheni ya vikosi kadhaa vya jeshi la nchi hiyo katika mji mkuu Abuja.

Amesema wanajeshi wa serikali wamefanikiwa 'kusafisha' vijiji vya Kawu na Ido viungani mwa Abuja, na kuwaangamiza magaidi 30, mbali na kusambaratisha maficho yao kwenye operesheni hiyo iliyopewa jina la 'Whirl Punch.'

Meja Jeneral Onyeuko ameeleza kuwa, jeshi la nchi kavu la nchi hiyo limefanikiwa kutwaa silaha zilizokuwa zikitumiwa na magaidi hao zikiwemo bunduki aina ya AK47, mkoba wa risasi, bunduki za rashasha na pikipiki sita.

Wanachama wa Boko Haram

Katika hatua nyingine, askari sita wa jeshi la Nigeria wameuawa katika shambulio la wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram usiku wa kuamkia jana Ijumaa.

Magaidi hao walishambulia kituo cha upekuzi katika mji wa Madalla katika barabara kuu ya Abuja-Kaduna jimboni Niger, na kuua askari sita na kujeruhi wengine kadhaa.

Genge hilo la ukufurishaji limedai kuwa shambulio hilo ni hujuma ya kulipiza kisasi cha kuuawa wanachama wake 30.

Tags