Jul 30, 2022 10:25 UTC
  • Waziri auawa katika shambulio la al-Shabaab msikitini Somalia

Waziri wa Sheria wa jimbo la Kusini Magharibi mwa Somalia, Hassan Ibrahim Lugbur pamoja na mtoto wake wa kiume ni miongoni mwa watu kadhaa waliouawa katika shambulio la kundi la kigaidi la al-Shabaab lililolenga waumini waliokuwa wamekusanyika msikitini kwa ajili ya Swala mjini Baidoa, kusini mwa nchi.

Watu wasiopungua 11 akiwemo mtoto mwingine wa kiume wa waziri huyo wamejeruhiwa kwenye shambulio hilo la jana Ijumaa mjini Baidoa, yapata kilomita 245 kusini magharibi mwa mji mkuu Mogadishu.

Genge la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda limetangaza kuhusika na hujuma hiyo, ambayo imejiri chini ya saa 48 baada ya kundi hilo la kitakfiri kufanya mashambulizi pacha kusini mwa Somalia.

Duru za habari zinaarifu kuwa, gaidi aliyekuwa amejifunga bomu alimlenga waziri huyo akitoka msikitini baada ya kuswali Swala ya Ijumaa na kisha kujiripua pembeni yake.

Magaidi wa al-Shabaab

Waziri Mkuu wa Somalia, Hamza Abdi Barre sanjari na kulaani hujuma hiyo ya kigaidi, ametuma salamu za rambirambi kwa familia na jamaa za wahanga wa shambulio hilo.

Meya wa mji wa Merca, makao makuu ya eneo la Lower Shabelle, Abdullahi Ali Wafow ni miongoni mwa watu 20 waliouawa katika miripuko miwili ya mabomu siku ya Alkhamisi kusini mwa nchi; mashambulizi ambayo al-Shabaab ilikiri pia kuhusika nayo.

 

 

 

Tags