Aug 05, 2022 01:13 UTC
  • Afrika Kusini yaripoti kifo cha kwanza kilichosababishwa na chanjo ya Corona

Afrika Kusini jana Alkhamisi ilitangaza habari ya kuaga dunia mtu mmoja baada ya kupigwa chanjo cha kukabiliana na maradhi ya Covid-19 ya Johnson and Johnson ya Marekani.

Profesa Hannelie Meyer, mwanasayansi mwandamizi katika Wizara ya Afya ya Afrika Kusini amesema muda mfupi baada ya mtu huyo kupigwa chanjo ya Johnson and Johnson, alipatwa na matatizo ya kiafya inayofahamika kama Guillain-Barre Syndrome, ambapo mfumo wa kinga hushambulia mfumo wa neva.

Afisa huyo wa Wizara ya Afya ya Afrika Kusini amesema baada ya mtu kukumbwa na hali hiyo, alilazimika kuwekwa kwenye mashine ya kupumilia, na muda mfupi baadaye akaaga dunia.

Profesa Meyer ameeleza kuwa, hakuna ugonjwa mwingine uliopatikana kwenye mwili wa mgonjwa huyo baada ya kupigwa chanjo, na kwa msingi huo inahesabiwa kuwa amefariki dunia kutokana na athari za chanjo hiyo.

Mwaka jana, Marekani ilisitisha kwa muda matumizi ya chanjo hiyo ya virusi vya Corona ya Johnson and Johnson, baada kuripotiwa kusababisha kuziba kwa mishipa kama matokeo ya tatizo la kuganda damu kwa baadhi ya watu waliopewa chanjo hiyo.

Aidha mwaka jana nchi kadhaa za Ulaya zilisimamisha matumizi ya chanjo ya kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 ya AstraZeneca kutokana na madhara yake kwa damu za watu waliopigwa chanjo hiyo.

Hata hivyo Shirika la Afya Duniani (WHO) limekuwa likisisitiza juu ya umuhimu wa watu wote kuchanjwa dhidi ya Corona, kwani faida za chanjo zenyewe ni nyingi ikilinaginishwa na madhara yake.

Tags