Aug 05, 2022 11:27 UTC
  • Rais Kiir na Machar warefusha kipindi cha mpito Sudan Kusini kwa miaka 2

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na makamu wake ambaye wamekuwa wakivutana na kuhitalifiana kwa muda mrefu sasa Riek Machar wametangaza kuwa wataendelea kuiongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa miaka miwili zaidi, mara tu kipindi cha mpito kitakapomalizika.

Hayo yametangazwa na Martin Elia Lomuro, Waziri anayesimamia masuala ya Baraza la Mawaziri wakati akihutubia waandishi wa habari akiwa mbele ya Kiir na Machar na kuongeza kuwa: Ramani mpya ya njia imebuniwa.

Ameeleza kuwa, wawili hao wamefikia makubaliano hayo ya kurefusha kipindi cha kusalia uongozini ili pande mbili ziweze kujadili changamoto na vizingiti vinavyozuia kutekelezwa makubaliano ya amani.

Hata hivyo wakosoaji wa muafaka huo wanasema wawili hao wameamua kujiongezea muda wa kubakia madarakani bila kushauriana na asasi za kiraia, makundi ya kisiasa na jamii ya kimataifa.

Rais Kiir na Machar

Sudan Kusini ilipaswa kuhitimisha kipindi cha mpito kwa kufanya uchaguzi mnamo Februari mwaka ujao 2023, lakini serikali hiyo ya umoja wa kitaifa imeshindwa kutekeleza vipengee muhimu vya makubaliano hayo, ikiwemo kuandaa rasimu ya katiba.

Makubaliano mapya ya amani katika taifa hilo changa zaidi barani Afrika yalifikiwa mwaka 2018, na kuhitimisha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano, na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 400,000.

 

Tags