Aug 06, 2022 03:53 UTC
  • Asasi za kiraia Tunisia zatilia shaka matokeo ya kura ya maoni

Asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya serikali nchini Tunisia yametilia shaka uhalali wa matokeo ya kura ya maoni ya kubadilisha katiba iliyofanyika zaidi ya wiki moja iliyopita.

Asasi hizo zimeitaka Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo (ISIE), kuchapisha data za kura hiyo, ili zifanye tathmini ya kubaini iwapo mchakato wa zoezi hilo ulikuwa na itibari au la.

Baadhi ya mashika hayo yameenda mbali zaidi na kuitaka tume hiyo ya uchaguzi kuhesabu upya kura za zoezi hilo lililofanyika Julai 25 mwaka huu.

Shirika la kupambana na ufisadi la 'I Watch' limewatuhumu maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo (ISIE) kwa utepetevu na kukosa itibari na maadili.

Hata hivyo Rais wa kamisheni hiyo ya uchaguzi, Farouk Bouasker amewakosoa vikali wanaodai kuwa zoezi hilo halikuwa huru na la haki, na ametishia kuwachukulia hatua za kisheria kwa kibua madai hayo bila kutoa ushahidi.

Watunisia katika maandamano ya kupinga kura ya maoni ya katiba iliyofanyika Julai 25

Maafisa wa uchaguzi Tunisia walisema asilimia 92.3 ya washiriki walipiga kura ya 'Ndio' kuunga mkono rasimu ya katiba mpya iliyopendekezwa na Rais Kais Saeid.

Kati ya watu milioni 9.2 waliojiandikisha kupiga kura nchini Tunisia, ni asilimia 27.5 pekee walijitokeza kushiriki katika zoezi hilo la kura ya maoni ya katiba.

Tunisia iko kwenye mgogoro mkubwa wa kisiasa tangu Julai 25, 2021, baada ya Rais Kais Saied kuvunja serikali, kusimamisha bunge na kutwaa mamlaka yote ya nchi.

 

Tags