Aug 06, 2022 08:01 UTC
  • Uchaguzi Kenya: Kampeni zamalizika leo baada ya wanasiasa kunadi sera zao

Leo Jumamosi 6, saa 12 jioni ndiyo siku ya mwisho ya kampeni na mikutano yote ya kisiasa nchini Kenya huku wananchi wakisubiri kwa hamu uchaguzi wa Jumanne.

Wagombea wote wanne wa urais nchini Kenya wamekuwa wakinadi sera zao katika mikutano yao na leo kunafanyika mikutano miwili mikubwa ya kampeni mjini Nairobi.

Wagombea wawili wakuu wa urais, Naibu wa Rais William Ruto wa Muungano wa Kenya Kwanza, na waziri mkuu wa zamani Raila Odinga wa Muungano wa Azimio leo wana mikutano yao ya mwisho ya kampeni mjini Nairobi. Ruto atahutubia wafuasi wake katika Uwanja wa Nyayo, naye Raila Odinga atakuwa katika Uwanja wa Kasarani. Rais Uhuru Kenyatta ambaye anamaliza kipindi chake cha mihula miwili na anamuunga mkono Odinga, atahutubu maeneo kadhaa katika eneo la Mlima Kenya, ambalo ni ngome yake ya kisiasa.

Jumanne  wananchi wa Kenya watashiriki katika uchaguzi wa kumchagua rais mpya, wabunge, maseneta, wawakilishi wa wanawake, magavana wa kaunti na wajumbe wa mabunge ya kaunti.

Uchaguzi wa Kenya unaotarajiwa kugharimu dola bilioni 3 katika matumizi ya jumla umetajwa kuwa ghali zaidi barani Afrika kwa msingi wa gharama ya dola 17 kwa kila mpiga kura.

Wagombea urais Kenya na umashuhuri wao 

Uchunguzi wa maoni uliofanya na aghalabu ya mashirika unaonyesha kuwa Raila Odinga anamuongoza William Ruto ingawa yamkini uchaguzi ukaingia duru ya pili. Kwa mujibu wa sheria ya Kenya mshindi ni lazima apate zaidi ya asilimia 51 ya kura zote na pia ni lazima pia apate asilimia 25 ya kura zilizopigwa katika kaunti 24 la sivyo uchaguzi utaingia duru ya pili.

Kuna jumla ya wapiga kura 22,120,458 ambao wamesajiliwa kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu.