Aug 06, 2022 10:53 UTC
  • Uganda yalisimamisha shirika linalotetea vitendo vya ufuska

Serikali ya Uganda imesimamisha shughuli za shirika moja lisilo la kiserikali linalotetea eti haki na maslahi ya mabaradhuli na walioko kwenye mahusiano ya watu wenye jinsia moja.

Stephen Okello, Mkuu wa Taasisi ya Kudhibiti Asasi Zisizo za Serikali Uganda amesema shirika hilo la Sexual Minorities Uganda (SMUG) limefungiwa kutokana na kuendesha shughuli zake kinyume cha sheria na bila kibali cha serikali.

Okello amesema, shirika hilo la SMUG limekuwa likifanya kazi pasi na kuwa na leseni yenye itibari ya kuiruhusu kuendeleza shughuli zake katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Uganda kama aghalabu ya nchi za Afrika, ni taifa la kihafidhina na lenye kufuata maadili ya kidini. Bunge la Uganda huko nyuma lilipasisha sheria ya kutilia mkazo na kulipa nguvu suala la kutokomeza vitendo vya ushoga na mahusiano ya watu wenye jinsia moja katika nchi hiyo.

Sheria hiyo iliweka adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa baadhi ya uhalifu unaohusiana na vitendo hivyo vya ufuska. Hata hivyo sheria hiyo ilibatilishwa na mahakama iliyosema kuwa ilipasishwa bila akidi katika Bunge la nchi hiyo.

Hii ni katika hali ambayo, baadhi ya Wabunge na viongozi wa kidini na kiraia wameapa kuuwasilisha upya muswada wa sheria hiyo ya kukabiliana na ushoga nchini humo.

Rais Yoweri Museveni wa nchi hiyo amewahi kunukuliwa akisema kuwa, ushoga katika nchi za Afrika ni nembo ya 'ubeberu wa kijamii' wa Wamagharibi. 

Tags