Aug 06, 2022 10:56 UTC
  • Wataalamu wa UN: Askari 'wazungu' walihusika na mauaji ya raia 33 Mali

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesema vikosi vya jeshi la Mali vilishirikiana na 'askari wazungu' katika operesheni iliyopelekea makumi ya raia kuuawa karibu na mpaka wa Mauritania mnamo Machi mwaka huu.

Shirika la habari la Associated Press limenukuu ripoti ya wataalamu wa UN ikisema kuwa, raia 33 waliuawa katika operesheni hiyo ya Machi 5 iliyovishirikisha vikosi vya Mali na wanajeshi waliotajwa kuwa weupe katika mji wa Robinet El Ataye, eneo la Segou, mpakani na Mauritania.

Ripoti hiyo haijaeleza uraia wa wanajeshi hao, lakini mara nyingi ripoti za aina hii za wataalamu wa UN zimekuwa zikiwaelekezea kidole cha lawama 'mamluki wa Russia' zinapotaja wanajeshi weupe. Russia imekunusha mara kadhaa kuwa na mamluki nchini Mali.

Ikumbukwe kuwa, mwezi uliopita wa Julai baada ya kushtadi mvutano kati ya Ufaransa na Mali, hatimaye Paris ilitangaza ukomo wa kuwepo kwa vikosi vya askari wa nchi za Ulaya vinavyojulikana kama Takuba, nchini Mali.

Wanajeshi wa Ufaransa wakiondoka Mali

Vikosi vya jeshi la Ufaransa vimekuwepo nchini Mali kwa takriban miaka 10 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Maafisa wa serikali ya Mali wanawatuhumu wanajeshi wa Ufaransa kuwa wanashirikiana na makundi ya kigaidi yanayotaka kujitenga eneo la kaskazini mwa nchi hiyo, kufanya ukatili dhidi ya raia na kushindwa kukabiliana ipasavyo na makundi ya kigaidi.

Takwimu za Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali zinaonesha kuwa, raia 543 wameuawa huku wengine 269 wakijeruhiwa katika miezi 3 ya kwanza ya mwaka huu. 

Tags