Aug 08, 2022 07:20 UTC
  • Magaidi wavamia vijiji na kuua watu 20 mashariki ya DRC

Makumi ya watu wameuawa katika mashambulio yaliyofanywa na genge moja la kigaidi huko mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Shirika la habari la Reuters limenukuu duru za kijeshi na asasi za kirai zikisema kuwa, watu wasiopungua 20 wameuawa huku wengine wengine wakijeruhiwa, baada ya magaidi kuvamia vijiji viwili mashariki ya DRC.

Inashikuwa kuwa, kundi la wapiganaji wa ADF ambalo ni moja ya makundi 120 ya wanagambo yanayoteteresha hali ya usalama na uthabiti mashariki ya Kongo DR, ndilo lililohusika na mauaji hayo ya wanavijiji 20.

Ijumaa iliyopita, kundi hilo la wanamgambo lilivamia kijiji cha Kandoyi katika mkoa wa Ituri mashariki ya DRC na kuua watu 10, na kujeruhiwa wengine kadhaa.

Wanajeshi DRC

Siku iliyofuata ya Jumamosi, mapigano makali yalijiri baina ya waasi hao na wanajeshi wa DRC katika kijiji hicho cha Kandoyi. Dieudonne Malangay, mwakilishi wa shirika la kiraia amesema raia mmoja aliuawa katika makabiliano hayo.

Kundi la waasi la ADF linalotokea kaskazini mashariki mwa Uganda limekuwa likiendesha shughuli zake katika maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa DRC tangu muongo wa 90, ambapo limeua mamia ya watu, na kupelekea malaki ya wengine kuwa wakimbizi.

 

Tags