Aug 08, 2022 07:28 UTC
  • AU yalaani ukatili wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza

Umoja wa Afrika (AU) umeungana na jamii ya kimataifa kulaani jinai za kinyama zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Ukanda wa Ghaza huko Palestina.

Katika taarifa jana Jumapili, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU, Moussa Faki Mahamat amesema kushambuliwa raia na kuendelea kukaliwa kwa mabavu maeneo ya Palestina na vikosi vya usalama vya Israel kinyume cha sheria kunakanyaga wazi sheria za kimataifa.

Taarifa hiyo imeeleza bayana kuwa, ukiukaji huo wa sheria za kimataifa unaofanywa na utawala wa ghasibu wa Israel unazidisha ugumu katika jitihada za kutafuta haki na suluhu ya kudumu.

Kabla ya hapo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini ilitoa taarifa rasmi ya kulaani jinai za Israel huko Gaza na kusema kuwa, jamii ya kimataifa ina wajibu wa kudhamini usalama wa raia wa Palestina kama zinavyosema sheria za kimataifa.

Unyani usio na kifani wa Wazayuni dhidi ya wakazi wa Gaza

Taarifa ya wizara hiyo imesisitiza kuwa, dunia inapaswa kuchukua hatua za kweli za kuulazimisha utawala vamizi wa Kizayuni ukomeshe mashambulizi yake dhidi ya raia hususan wanawake na watoto wadogo wa Ukanda wa Gaza.

Malaysia na Uturuki pia zimetoa taarifa za kulaani mashambulio ya kinyama ya utawala dhalimu wa Kizayuni, ambayo hadi sasa yamepelekea kuuawa shahidi Wapalestina zaidi ya 40, na mamia ya wengine wamejeruhiwa.

Tags