Aug 08, 2022 11:41 UTC
  • Maafisa tano wa Polisi Mali wauawa katika hujuma ya kigaidi

Watu wanaoaminika kuwa ni magaidi waliwaua maafisa watano wa polisi nchini Mali siku ya Jumapili kusini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika

Hujuma hiyo imejiri wakati jeshi la Mali limetangaza kukabiliana na  magaidi wakufurishaji kaskazini mashariki mwa nchi hiuo.

Idara ya Polisi ya Mali imesema kikosi cha doria cha kituo cha polisi cha Sona kilikanyaga kilipuzi na baada ya hapo kukajiri ufyatulianaji mkali wa risasi uliofanywa na washambuliaji.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa “maafisa watano wa polisi waliuawa, mmoja akajeruhiwa na washambuliaji wengine watatu wakatoweka.”

Shambulio hilo lilifanyika katika mji wa Sona, katika eneo la Koutiala, karibu na mpaka kati ya Mali na Burkina Faso.

Afisa wa Polisi ambaye hakutaka jina lake litakwe amesema washambuliaji walikuwa magaidi.

Wanajeshi wa Mali

Magaidi wa makundi ya ukufurishaji yanayofungamana na ISIS au al-Qaeda wamekuwa wakitekeleza mashambulizi dhidi ya raia na walinda amani wa Umoja wa Mataifa kwa muda mrefu sasa katika nchi ya Mali na nchi nyingine za eneo la Ziwa Chad, magharibi mwa Afrika.

Mgogoro wa hali mbaya ya kiusalama umeigubika Mali tangu mwaka 2012; na vikosi vya majeshi kutoka nje hasa vya Ufaransa vilivyotimuliwa hivi karibuni havijaweza kurejesha amani na usalama katika nchi hiyo.