Aug 08, 2022 11:57 UTC
  • Waangalizi 18,000 wa ndani, na kimataifa kufuatilia mchakato wa uchaguzi Kenya

Waangalizi 18,000 wanatarajiwa kufuatilia uchaguzi mkuu wa Kenya utakaofanyika kesho Jumanne.

Wafula Chebukati, mkuu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) amesema tume hiyo ndiyo ambayo imetoa vibali kwa waangalizi hao.

Serikali ya Kenya imetangaza kuwa kesho Jumanne Agosti 9 itakuwa siku ya mapumziko kitaifa ili kuwawezsha wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

Kuna zaidi  ya vituo 46,200 vya kupigia kura kote katika nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi Afrika Mashariki huku idadi ya wapiga kura waliojisajili ikiwa ni takaribani milioni 22 waliojiandikisha nchini humo kati ya milioni 54.

Katika uchaguzi wa kesho Wakenya wanatazamiwa kumchagua rais mpya, wajumbe wa baraza la seneti, wajumbe wa bunge la kitaifa, wawakilishi wa wanawake bungeni, magavana wa kaunti zote 47 na wawakilishi wa mabunge ya kaunti.

Baada ya kuhudumu kwa mihula miwili ya juu iwezekanavyo, Uhuru Kenyatta haruhusiwi kisheria kushiriki kwenye kinyang'anyiro cha urais.

Mchuano wa karibu unatarajiwa kuwa kati ya wagombea wawili wakuu - William Ruto, naibu rais wa Kenya tangu 2013 na kiongozi wa Muungano wa Kenya Kwanza, na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.

Rais Uhuru Kenyatta

Kenyatta ameamua kumuunga mkono Odinga, mpinzani wake wa zamani kwa wadhifa huo mkuu ambaye anagombea urais mara ya tano, badala ya makamu wake mwenyewe.

Kenya ilikabiliwa na miezi kadhaa ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2017 ambazo zilipelekea makumi ya watu kuuawa. Ghasia hizo zilisita baada ya Rais Kenyatta kufikia mapatnao na hasimu wake Raila Odinga. Mapatano hayo yalipelekea kuzorota uhusiano wa Kenyatta na naibu wake, William Ruto.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na aghalabu ya mashirika unaonyesha kuwa Raila Odinga anamuongoza William Ruto ingawa yamkini uchaguzi ukaingia duru ya pili. Kwa mujibu wa sheria ya Kenya mshindi ni lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zote na pia ni lazima apate asilimia 25 ya kura zilizopigwa katika kaunti 24 la sivyo uchaguzi utaingia duru ya pili.