Aug 09, 2022 03:16 UTC
  • Askari wa Nigeria washambulia Waislamu waliokuwa kwenye maombolezo ya Ashura

Askari wa serikai ya Nigeria wameshambulia kumbukuku za maomboleza ya Ashura ya Imam Husain AS katika mji wa Zaria na kuua shahidi na kujeruhi Waislamu kadhaa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, askari wa Nigeria jana Jumatatu waliwashambulia Waislamu hao waliokuwa katika kumbukumbu za siku ya kuuawa shahidi Imam Husain AS katika mji huo wa Zaria wa jimbo la Kaduna la kaskazini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Mmoja wa watu walioshuhudia aliyejitambulia kwa jina la Abdulhakam Muhammad amesema kuwa, Waislamu walikuwa katikati ya maombolezo ya Ashura, wakati askari wa serikali walipoanza kuwashambulia baada ya Sala ya Adhuhuri hiyo jana.

Waislamu wa Kishia mjini Zaria Nigeria, hawasalimiki hata kidogo na ukandamizaji wa askari wa Serikali

 

Shuhuda huyo amesema pia kuwa amemuona kwa macho yake kijana mmoja mdogo akiuawa shahidi kwa risasi za askari hao ingawa watu wengi walianza kukimbia baada ya askari wa Nigeria kuwafyatulia risasi.

Shuhuda mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Abu Haidar Zaria ameliambia shirika la habari la Iran Press kwamba kuna uwezekano idadi wa Waislamu waliouawa shahidi kwenye shambulio hilo wakawa ni wengi kwani polisi wamefanya haraka kuondoa majeruhi na watu waliopigwa risasi.

Jana Jumatatu ilisadifiana na mwezi 10 Mfunguo Nne Muharram ambayo ni maarufu kwa jina la Siku ya Ashura ya kuuawa shahidi kikatili mjukukkuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW katika jangwa la Karbala la Iraq ya leo mwaka 61 Hijria.

Siku hii ni muhimu sana kwa Waislamu wa madhehebu ya Kishia na wapenzi wa Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW kote duniani.

Tags