Aug 09, 2022 10:59 UTC
  • Wananchi wa Morocco wateketeza moto bendera za Israel katika maandamano

Wananchi wa Morocco waliokuwa na hasira wameteketeza moto bendera za utawala wa Kizayuni wa Israel mbele ya bunge la nchi hiyo katika maandamano ya kulaani hujuma ya utawala huo dhidi ya Gaza.

Aidha wameteketeza moto bendera hizo za utawala wa Kizayuni kama njia ya kulaani hatua ya utawala wa Morocco kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo. Mnamo Disemba mwaka 2020, Morocco na utawala wa Kizayuni wa Israel zilitangaza kuanzisha uhusiano wa kawaida katika mapatano yaliyosimamiwa na Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa, Wamorocco wamekusanyika nje ya bunge la nchi hiyo huku wakipiga nara za kutaka nchi yao isitishe mchakato wa uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizyuni wa Israel.

Maandamano hayo yameandaliwa na harakati za Kiislamu na vyama vya mrengo wa kushoto nchini Morocco.

Waandamanaji wamelaani vikali hujuma ya hivi karibuni ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza ambapo Wapalestina 45 wameuawa shahidi wakiwemo watoto 15.

Mfalme wa Morocco

Kati ya nara zilizopigwa na waandamanaji ni pamoja na  "Wananchi wanataka kusitishwa uhusiano wa kawaida na Israel" na "Palestina ni Amana, Uhusiano na Israel ni Uhaini." Waandamanaji hao waliokuwa na hasira pia wameteketeza moto bendera za Israel.

Baada ya kufikiwa mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina ya Israel na ufalme wa Morocco, pande mbili zimeimarisha maingiliano ambapo maafisa wa ngazi za juu wa Israel wametembelea Morocco na kutia saini mikataba ya ushirikiano wa kijeshi, kiuchumi, kimchezo na kifilamu. Wananchi wa Morocco wametangaza azma yao ya kuendelea kupinga uhusiano na Israel na kuunga mkono wananchi wa Palestina.

Tags