Aug 10, 2022 08:03 UTC
  • UN: Tunahitaji dola milioni 73 kuwasaidia kwa chakula wakimbizi wa ndani Ethiopia

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa na serikali ya Ethiopia wametoa ombi la kupatiwa dola milioni 73 ili kuweza kuendelea na utoaji msaada wa chakula kwa wakimbizi 750,000 walioko nchini humo katika kipindi cha miezi sita ijayo.

Taarifa kutoka Addis Ababa nchini Ethiopia imeyataja mashirika hayo kuwa ni lile la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP na linalohudumia wakimbizi UNHCR  yanayoshirikiana na lile la serikali ya Ethiopia la kuhudumia wakimbizi na waliorejea kutoka ughaibuni RRS. 

Taarifa hiyo imefafanua kuwa ifikapo mwezi Oktoba WFP haitakuwa na chakula kabisa hali itakayoziacha maelfu ya familia katika hali ya hatari kwa kuwa zinategemea chakula hicho cha msaada ili kuweza kuishi. 

Mwakilishi wa WFP nchini Ethiopia Claude Jibidar amesema “robo tatu ya wakimbizi wataachwa bila chakula ufadhili usipopatikana mara moja. Kuendelea kukatwa kwa fedha kunatuweka kwenye wasiwasi maana wakimbizi wengi wanaweza kufikiria kurejea katika maeneo yao ya asili ambayo si salama.”

 

Mkuu huyo wa WFP anawasiwasi huo kutokanaa na ukweli kwamba kupunguzwa kwa mgao wa chakula nchini humo kulianza mwezi Novemba 2015 kwa asilimia 15, mwezi Novemba 2021 chakula kilipunguzwa kwa asilimia 40 na mwezi Juni mwaka huu 2022 mgao huo umepunguzwa mpaka asilimia 50.

Ethiopia inawahifadhi wakimbizi na wasaka hifadhi zaidi ya milioni moja. Wengi wao wanatoka nchi za Sudan Kusini, Somalia, Eritrea na Sudan. Kati ya wakimbizi hao, takriban 750,000 wanategemea moja kwa moja msaada wa chakula unaotolewa na mashirika ya kibinadamu.../

Tags