Aug 10, 2022 15:13 UTC
  • Ruto aongoza katika matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais Kenya

Mgombea wa kiti cha rais wa chama cha UDA katika uchaguzi mkuu nchini Kenya, William Ruto anaongoza katika matokeo ya muda ya zoezi hilo la kidemokrasia lililofanyika jana Jumanne.

Kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyochapishwa kwenye tovuti ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini humo IEBC yanaonesha kuwa, Ruto anaongoza kwa asilimia 52 ya kura.

Yuko mbele ya Raila Odinga ambaye anawania kiti hicho kwa chama cha Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, ambaye ameambulia asilimia 46 ya kura zilizohesabiwa kufikia sasa.

Ruto ambaye ni Naibu Rais na kinara wa Muungano wa Kenya Kwanza amezoa kura zaidi ya milioni 3 hadi tunaingia mitamboni, huku Odinga ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu akipata milioni 2.7.

Saa chache zilizopita Odinga alikuwa anaongoza kwenye mchuano huo mkali kati yake na Ruto

Tume hiyo inakadiria kuwa asilimia 60 ya wapiga kura milioni 22.1 waliojiandikisha wametumia haki zao za kidemokrasia katika uchaguzi mkuu ambao unafuatiliwa na waangalizi 18,000 wakiwemo waangalizi 1,300 wa kimataifa.

Wapiga kura walipiga kura kwa ajili ya kuchagua rais, magavana, wabunge wa seneti na bunge la kitaifa, wawakilishi wa wanawake katika bunge la kitaifa na wajumbe wa mabunge ya kaunti.

Tags