Aug 11, 2022 02:56 UTC
  • Odinga ampiku Ruto; Wakenya waendelea kusubiri kwa hamu matokeo ya urais

Raila Odinga ambaye anagombea kiti rais katika uchaguzi mkuu nchini Kenya kwa chama cha Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, yupo kifua mbele katika matokeo ya muda, saa chache baada ya mpinzani wake wa karibu anayewania kwa chama cha UDA, William Ruto kuongoza katika matokeo ya awali ya zoezi hilo lililofanyika Jumanne.

Kwa mujibu wa matokeo ya awali ya uchaguzi huo wenye mchuano mkali yaliyochapishwa kwenye tovuti ya gazeti la Daily Nation, Odinga anaongoza kwa asilimia 51 ya kura zilizohesabiwa kufikia sasa.

Ruto ambaye ni Naibu Rais mwenye umri wa miaka 55 ameambulia asilimia 48 ya kura zilizohesabiwa hadi tunaingia mitamboni.

Ruto ambaye pia ni kinara wa Muungano wa Kenya Kwanza na ambaye anawania kiti cha rais kwa mara ya tano sasa amezoa kura zaidi ya milioni 4.7 hadi sasa, huku Odinga ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki akipata kura zaidi ya milioni 5.

George Wajackoyah wa chama cha Roots mpaka sasa ameambulia kura 44,000, sawa na asilimia 0.45 ya kura zilizohesabiwa, akifuatiwa na David Waihiga wa chama cha Agano ambaye amepata kura 22,000 hadi sasa.

Kwa mujibu wa matokeo hayo ya muda, kura karibu milioni 10 kutoka vituo 31,000 kati ya 46,000 zimehesabiwa kufikia sasa, matokeo ambayo yanabadilika ndani ya kila dakika kadri kura zinavyozidi kuhesabiwa.

Uchaguzi Kenya

Tume ya Uchaguzi Kenya IEBC inakadiria kuwa asilimia 60 ya wapiga kura milioni 22.1 waliojiandikisha wametumia haki zao za kidemokrasia katika uchaguzi mkuu ambao unafuatiliwa na waangalizi 18,000 wakiwemo waangalizi 1,300 wa kimataifa.

Wakenya wanaendelea kusubiri kwa hamu na shauku kuu matokeo rasmi ya mwisho ya uchaguzi wa rais, huku baadhi ya matokeo ya ugavana, useneta, ubunge na udiwani yakiwa tayari yameshatangazwa.

Tags