Aug 11, 2022 07:37 UTC
  • Mahakama Tunisia yatengua uamuzi wa rais kuwatimua majaji

Mahakama moja nchini Tunisia imebatilisha uamuzi wa Rais Kais Saied wa nchi hiyo wa kuwafuta kazi makumi ya majaji.

Imad Al-Ghabri, Msemaji wa Mahakama ya Utawala nchini humo amesema korti hiyo imepitia rufaa zote zilizowasilishwa dhidi ya uamuzi huo wa rais, na kuamua kusitisha utekelezaji wake.

Murad al-Masoudi, Kiongozi wa Jumuiya ya Majaji Vijana amesema rufani 47 ziliwasilishwa na majaji waliofukuzwa kazi kupinga uamuzi huo uliochukuliwa na Rais Kais Saied mwezi Juni mwaka huu. 

Rais huyo alitangaza kuwafuta kazi majaji 57, akiwatuhumu kuhusika na ufisadi na eti kuwapa himaya magaidi. Makundi ya kisiasa na mashirika ya kiraia nchini humo, pamoja na asasi za kimataifa za kutetea haki za binadamu zilikosoa vikali uamuzi huo.

Vyama vya kisiasa vinamtaka Rais Kais Saied kuachia ngazi na kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi mkuu wa mapema nchini humo.

Rais Kais Saied 

Haya yanajiri wiki chache baada ya asilimia 92.3 ya washiriki wa kura ya maoni kupiga kura kuunga mkono rasimu ya katiba iliyopendekezwa na Rais Saied. Bodi ya uchaguzi nchini humo, hata hivyo, ilisema waliojitokeza kupiga kura ni 27.5% pekee ya wapiga kura waliostahili.

Tunisia iko kwenye mzozo mkubwa wa kisiasa tangu Julai 25 mwaka jana 2021, wakati Saied alipoivunja serikali, kusimamisha bunge na kutwaa mamlaka yote ya nchi.

Tags