Aug 11, 2022 07:43 UTC
  • Watu 8 wauawa, wafungwa 800 watoroka jela DRC

Watu wanane wakiwemo askari polisi wawili na raia mmoja wameuawa katika shambulio la kigaidi la wapiganaji wa ADF kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kapteni Anthony Mualushayi, Msemaji wa Jeshi la Kongo DR amesema magaidi wa ADF usiku wa kuamkia jana walivamia Gereza la  Kakwangura mjini Butembo katika mkoa wa Kivu Kaskazini kwa lengo la kuwatorosha wanachama wenzao 13, wakiwemo wanawake 12.

Amesema jeshi la DRC liliingilia kati kuzima shambulio hilo lakini kwa kuchelewa. Vyombo vya habari vya Kongo DR vimesema mbali na watu wanane kuuawa kwenye makabiliano hayo, wafungwa zaidi ya 800 wamefanikiwa kutoroka jela.

Genge la ADF limefanya hujuma hiyo siku chache baada ya wanachama wake kuvamia vijiji viwili mashariki ya DRC, na kuua watu wasiopungua 20.

Wanamgambo wa ADF-Nalu wa DRC

Kundi la wapiganaji wa ADF ambalo ni moja ya makundi 120 ya wanagambo yanayoteteresha hali ya usalama na uthabiti mashariki ya Kongo DR, Ijumaa iliyopita lilivamia kijiji cha Kandoyi katika mkoa wa Ituri mashariki ya DRC na kuua watu 10, na kujeruhiwa wengine kadhaa.

Kundi la waasi la ADF linalotokea kaskazini mashariki mwa Uganda limekuwa likiendesha shughuli zake katika maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa DRC tangu muongo wa 90, ambapo limeua mamia ya watu, na kupelekea malaki ya wengine kuwa wakimbizi.

 

Tags