Aug 11, 2022 10:44 UTC
  • Katibu MKuu wa UN apongeza amani katika uchaguzi wa Kenya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewapongeza wananchi wa Kenya kwa kupiga kura kwa amani wakati wa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliofanyika hapo juzi Agosti 9, 2022

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Katibu Mkuu Stéphane Dujarric kutoka New York Marekani imesema Katibu Mkuu anatambua kazi muhimu iliyofanywa na mamlaka ya Kenya pamoja na mashirika mengine yote yanayohusika na usimamiz wa uchaguzi, ushirikishwaji wa wadau mbalimbali wa kitaifa na dhamira ya dhati isiyoyumbishwa ya wapiga kura kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura. 

“Katibu Mkuu ana imani wadau wote wa kisiasa na wananchi wa Kenya wataendelea kuonesha kiwango hicho hicho cha utulivu, subira na heshima kwa mchakato huo wa uchaguzi wakati huu wakisubiri kutangazwa matokeo ya kura kwa mujibu wa muda uliowekwa kisheria” amesema Dujarric.

Katibu Mkuu amesisitiza uwepo wa Umoja wa Mataifa kuendelea kuunga mkono juhudi zote zinazofanywa na mamlaka ya nchi hiyo na wananchi wote wa Kenya ili kuhakikisha wanaendeleza mchakato wa kidemokrasia nchini humo. 

Upigaji Kura nchini Kenya

Haya yanajiri huku Wakenya wakiendelea kusubiri kwa hamu matokeo ya kura ya urais baada ya uchaguzi wa Jumanne kumalizika kwa amani. Matokeo ya awali yanaonesha mchuano mkali baina ya naibu wa rais William Ruto na mwanasiasa mkongwe Raila Odinga. Maafisa wa tume huru ya uchaguzi na mipaka ya Kenya IEBC, wanaendelea na zoezi la kuhesabu kura.

Kwa mujibu wa sheria tume hiyo inapaswa kutangaza matokeo kufikia Agosti 16. Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amewatolea wito Wakenya kuwa watulivu, kuepuka madai ya udanganyifu wa kura ambayo yaligubika chaguzi zilizopita.

Kwa mujibu wa sheria ya Kenya mshindi wa urais ni lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zote na pia ni lazima apate asilimia 25 ya kura zilizopigwa katika kaunti 24 la sivyo uchaguzi utaingia duru ya pili.