Aug 12, 2022 02:23 UTC
  • Mali yatangaza siku 3 za maombolezo baada ya kuuawa makumi ya askari wake

Viongozi wa Mali wametangaza siku tatu za maombolezo ya nchi nzima kuanzia jana Alkhamisi baada ya kutokea mashambulio kadhaa yaliyoua makumi ya wanajeshi na maafisa wa polisi katika kona mbalimbali za nchi hiyo.

Shambulizi la uwagaji mkubwa zaidi wa damu ni lile lililotokea Jumapili iliyopita katika mji wa Gao wa kaskazini mwa Mali ambalo liliua wanajeshi 42 wa nchi hiyo. Taarifa zinasema kuwa, magaidi hao walitumia ndege zisizo na rubani na magari wakati wa shambulio hilo.

Katika sehemu nyingine, maafisa watano wa polisi wa serikali ya Mali waliuawa siku hiyo hiyo ya Jumapili baada ya magaidi kushambulia kituo cha polisi karibu na mpaka wa Mali na Burkina Faso.

Vitendo vya ukatili na kuchoma moto nyumba na mashamba vinatokea mara kwa mara nchini Mali

 

Mkurugenzi Mkuu wa polisi wa Mali, Soulaimane Traore, amethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, maafisa wengine watatu wa polisi hawajulikani walipo hadi hivi sasa tangu lilipotokea shambulio hilo la siku ya Jumapili kwenye mpaka wa Sona. 

Siku ya Jumatatu, genge la ukufurishaji liitwalo JNIM na ambalo lina mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida lilitangaza kuhusika na mashambulizi na mauaji hayo.

Kabla ya kutangazwa habari hii, mamlaka za Mali zilikuwa zimetangaza kuwa, mbali na kuuawa wanajeshi 42, wanajeshi wengine 22 wamejeruhiwa kwenye shambulizi hilo.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa, magaidi 37 waliangamizwa kwenye mapigano hayo baina ya genge la kigaidi na askari wa serikali ya Mali.