Aug 12, 2022 02:26 UTC
  • Buhari alemewa, hajui akabiliane vipi na machafuko ya Nigeria nzima

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ameemewa na kwa kweli hajui akabiliane vipi na machafuko yaliyoenea katika kona zote za nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika hususan maeneo yake ya kaskazini.

Hayo yameripotiwa na shirika la habari la AFP ambalo pia limeandika, ikiwa imebakia miezi sita tu hadi kufanyika uchaguzi wa rais nchini Nigeria, malalamiko dhidi ya Muhammadu Buhari (79) yamezidi kuwa makubwa.

Asilimia kubwa ya wananchi wa Nigeria wanaamini kuwa rais wao huyo hana uwezo wa kuleta utulivu na wala kukabiliana na magenge yanayotenda jinai dhidi ya wananchi.

Nigeria ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika na kwa miaka mingi sasa imekumbwa na wimbi zito la mauaji na machafuko.

Magenge ya kigaidi yanafanya jinai kubwa dhidi ya wananchi huko Nigeria

 

Shirika hilo la AFP limenukuu taarifa ya Kituo cha Demokrasia na Maendeleo cha Nigeria kikisema kuwa, hivi sasa kuna mashinikizo makubwa kutoka kwa matabaka yote ya wananchi wa nchi hiyo ya kutaka kudhaminiwa usalama wao na kupambana vilivyo na magenge yanayohatarisha amani na yanayofanya jinai dhidi ya wananchi.

Kituo hicho kimeongeza kuwa, tatizo kubwa la Nigeria hivi sasa ni kwamba hakuna mtu yeyote anayehisi kuwa yuko kwenye usalama. Yale magenge ya wanamgambo tuliyodhani kuwa yameishiwa nguvu ndio kwanza yanazidi kupata nguvu.

Mwezi uliopita, magaidi wa Daesh (ISIS) walivamia jela moja nje ya mji mkuu Abuja na kuwaachilia huru mamia ya wahalifu waliokuwa wamefungwa kwenye jela hiyo.