Aug 12, 2022 07:34 UTC
  • Waangalizi wa kimataifa wameridhishwa na uchaguzi Kenya

Waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi wamefurahishwa na uchaguzi wa Kenya na sasa wanatoa wito wa ukabidhianaji madaraka kwa amani.

Wakizungumza Alhamisi mjini Nairobi, waaangalizi walipongeza watu wa Kenya na tume ya uchaguzi kwa kuendesha uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika siku ya Jumanne.

Kufikia Alhamisi, bado kulikuwa na mbio za farasi wawili kati ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, 77, na Naibu Rais William Ruto, 56.

Kwa mujibu wa matokeo ya awali, kuna mchuano mkali baina ya wagombea wawili wa urais Raila Odinga wa Muugano wa Azimio na Ruto wa Muungano wa Kenya Kwanza na bado ni vigumu kutabiri ni yupi baina ya hao wawili ataibuka mshindi.

Rais wa zamani wa Tanzania Jakaya Kikwete, ambaye anaongoza Ujumbe wa Waangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ameuambia mkutano na waandishi wa habari mjini Nairobi kwamba, "tumeridhishwa na mchakato huo hadi sasa.“Tuna wasiwasi kuhusu uandikishwaji mdogo wa wapigakura vijana. Kinyume na matarajio ya wapiga kura vijana milioni 6, ni milioni 3 pekee waliojiandikisha. Hili linapaswa kuhusisha kila mtu kuwa vijana hawashiriki katika mchakato wa uchaguzi ," Kikwete alisema, huku akionyesha kusikitishwa na taarifa potofu za mitandao ya kijamii.

Ujumbe wa waangalizi wa EAC umewataka raia wa Kenya kuendelea kudumisha amani kwani nchi hiyo ya Afrika Mashariki bado inasubiri kukamilika mchakato wa uchaguzi.

Raila Odinga (kushoto) na William Ruto

Ujumbe wa waangalizi wa Mamlaka ya Kieneo ya Kiserikali ya Maendeleo ya Uangalizi wa Uchaguzi (IGAD) pia umeipongeza Kenya kwa uchaguzi uliofaulu. IGAD ni jumuiya ya kieneo yenye nchi wanachama ambazo ni Djibouti, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Uganda.

"IGAD inawapongeza watu wa Kenya kwa kujitolea na uvumilivu ambao wameonyesha katika uchaguzi wa Agosti 9," Katibu Mtendaji wa IGAD, Workneh Gebeyehu, ambaye alikuwa waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia kuanzia 2016 hadi 2019 amesema.

Mkutano huo wa waandishi habari pia ulihudhuriwa na waangalizi wa Umoja wa Afrika na Soko la Pamoja la Afrika Mashariki na Kati (COMESA).

Uchaguzi wa Kenya umekumbwa na idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza kihistoria, kulingana na tume ya uchaguzi nchini humo.

Shughuli ya upigaji kura nchini Kenya iliendeshwa katika vituo 46,229, na wananchi walipiga kura kwa ajili ya rais, magavana, wabunge wa bunge la kitaifa na seneti, wawakilishi wa wanawake na wajumbe wa mabunge ya kaunti.

Uchaguzi mkuu ulifuatiliwa na waangalizi 18,000 wakiwemo waangalizi 1,300 wa kimataifa.

Kwa mujibu wa sheria ya Kenya mshindi wa uraia ni lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zote na pia ni lazima apate asilimia 25 ya kura zilizopigwa katika kaunti 24 la sivyo uchaguzi utaingia duru ya pili.