Aug 12, 2022 07:57 UTC
  • Ethiopia yawasha mtambo wa pili kwenye bwawa la GERD katika Mto Nile

Ethiopia imewasha mtambo (turbine) wa pili wa Bwawa lake la Grand Ethiopian Renaissance (GERD), la kuzalisha umeme wa maji lenye thamani ya dola bilioni 5.

Siku ya Alhamisi Waziri Mkuu Abiy Ahmed aliwasha injini ya bwawa hilo kubwa zaidi barani Afrika hadi sasa, lililojengwa takriban kilomita 45 (maili 28) mashariki mwa mpaka na Sudan kwenye Blue Nile, mkondo mkuu wa Mto Nile.

Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance ambalo pia linajulikana kama  Al-Nahda limekuwa likijengwa tangu mwaka 2011 ili kuzalisha takriban megawati 6,000 za umeme kwa mwaka wakati mitambo yote 13 inafanya kazi, kulingana na serikali ya Ethiopia.

Tangu kuanzishwa kwake, kumekuwa suala la mzozo kati ya Misri na Ethiopia, huku Cairo ikieleza wasiwasi wake kwamba "sehemu yake ya kihistoria" ya maji ya Mto Nile itapungua, wakati Ethiopia inasema mradi huo ni muhimu kwa maendeleo yake ya kitaifa.

Bwawa hilo lenye urefu wa mita 145 na upana  wa mita 1,800, lina uwezo wa kushika mita za ujazo bilioni 70 za maji kwenye hifadhi yake.

Akizungumza jana, Abiy amesema bwawa hilo "ni mradi ambao Waethiopia wamewekeza kwa jasho, pesa, na wakati, na wengine maisha yao muhanga wakiwa wanatekekeleza majukumu ya kufanikisha mradi huo.

Wakati huo huo, mazungumzo ya pande tatu kuhusu bwawa hilo kati ya Ethiopia, Sudan, na Misri bado yamekwama.

Misri na Sudan zimeitaka Ethiopia kutia saini makubaliano "ya kisheria na kamili" juu ya kujaza maji na uendeshaji wa bwawa hilo, matakwa yaliyopingwa na Addis Ababa. Cairo inalitazama bwawa hilo kama tishio kwa sehemu yake ya maji ya Nile, chanzo chake pekee cha maji safi.

Ethiopia inaendelea kujaza hifadhi kwenye bwawa hilo kwa kutegemea tamko la 2015 ililotia saini na Khartoum na Cairo, ambapo Addis Ababa ina haki ya kuendelea na kazi za ujenzi wakati mazungumzo yanaendelea.

Mazungumzo kati ya nchi hizo tatu yamegonga mwamba baada ya kuendelea kwa miaka kadhaa.

Mwaka jana, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa wito kwa mataifa yote matatu kuanza tena mazungumzo yanayoongozwa na Umoja wa Afrika kuhusu mgogoro huo.

Ethiopia mwezi huu ilizindua hatua ya tatu ya kujaza bwawa hilo, licha ya upinzani kutoka Misri na Sudan.