Aug 12, 2022 08:02 UTC
  • Watu kadhaa wauawa katika maandamano Somaliland wakipambana na polisi

Watu kadhaa waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa siku ya Alhamisi baada ya polisi kuwafyatulia risasi waandamanaji wanaoipinga serikali katika miji kadhaa ya eneo lililojitenga la Somalia la Somaliland.

Mamia ya watu waliandamana mitaani katika mji mkuu Hargeisa na miji ya Burao na Erigavo baada ya mazungumzo kati ya serikali na vyama vya upinzani kuvunjika, huku upinzani ukiishutumu serikali kwa kutaka kuchelewesha uchaguzi wa rais mwezi Novemba.

Waandamanaji waliokuwa na hasira  walibeba mabango yaliyosema "Andaeni uchaguzi tarehe 13 Novemba 2022"  huku wakipiga nara dhidi ya serikali.

Abdirahman Mohamed Abdullahi, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Waddani, aliuambia umati wa watu huko Hargeisa kuwa, "Amani inaweza tu kuwepo katika Somaliland kwa uchaguzi wa haki na huru."

Katika mkutano na waandishi wa habari kiongozi huyo wa Waddani alishutumu serikali kwa kufanya "unyama" dhidi ya waandamanaji.

“Haya yalikuwa maandamano ya amani na tumeongoza watu waliobeba mabango na filimbi pekee, lakini serikali imefanya ukiukwaji kwa kutumia nguvu kubwa, risasi za moto na mabomu ya machozi,” amesema.

Uchaguzi  umepangwa kufanyika Novemba 13, lakini upinzani umeeleza wasiwasi wake kwamba serikali inajikokota kuhusu maandalizi.

Uamuzi wa serikali wa kusajili vyama vipya vya kisiasa kabla ya uchaguzi pia umekasirisha Waddani na chama kingine cha upinzani cha Haki na Ustawi (UCID) kwa hofu kwamba uwepo wa vyama vipya utaibua mifarakano katika upinzani.

Eneo la Somaliland ambalo lilikuwa koloni la  Uingereza kabla ya kujiunga na Somalia 1960 lilitangaza uhuru wake kutoka kwa Somalia mwaka 1991 lakini hatua hiyo haijatambuliwa na jumuiya ya kimataifa, na kuacha eneo la Pembe ya Afrika lenye takriban watu milioni likiwa limetengwa.

Somaliland hata hivyo imesalia kuwa tulivu huku Somalia ikikumbwa na miongo kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, ghasia za kisiasa na mashambulizi ya kundi la kigaidi la Al Shabab.