Aug 12, 2022 14:39 UTC
  • Tume ya Uchaguzi Kenya yakanusha madai ya kudukuliwa mfumo wake

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC) imepuuzilia mbali madai kuwa mfumo wake wa kuendesha uchaguzi umedukuliwa, huku Wakenya wakiendelea kusubiri kwa hamu na shauku kuu matokeo rasmi ya mwisho ya uchaguzi wa rais.

Akiongea na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Bomas jijini Nairobi leo Ijumaa, Ofisa Mkuu Mtendaji wa IEBC, Marjan Hussein Marjan amesema, "Kuna taarifa za upotoshaji kuwa tovuti ya matokeo imedukuliwa. Tunataka kulihakikishia taifa kuwa hakuna kitu kama hicho kimefanyika."

Amesisitiza kuwa, mfumo wa kuendesha uchaguzi ni madhubuti na wala hauwezi kudukuliwa. Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati amewalaumu maajenti wa vyama vya kisiasa kwa kusababisha utoaji wa matokeo ya urais kwa mwendo wa kinyonga.

Wakati huohuo, vyombo vya habari nchini humo vimeacha kupeperusha mubashara matokeo ya kura za urais, na hivyo kuzusha maswali kuhusu matokeo hayo katika kipindi hiki ambacho mchakato wa kuhesabu kura ukiingia siku yake ya nne.

Mchuano mkali ni baina ya Raila Odinga ambaye amegombea kiti rais kwa chama cha Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya na William Ruto aliyewania kwa chama cha UDA. Kufikia sasa wote wameambulia 49% ya kura zilizohesabiwa.

Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati

Tume ya IEBC imeendelea kusubiri fomu zilizotumiwa kuwatangaza washindi kwenye vituo vya kupigia kura. Fomu hizo zinazojulikana kama 34A, ndizo zinazohitajika, ili zikaguliwe sambamba na nakala zilizotumwa kwa kutumia vifaa vya KIEMS punde baada ya kura za urais kuhesabiwa Jumanne usiku.

Waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi wamefurahishwa na mchakato wa uchaguzi wa Kenya na sasa wanatoa wito wa ukabidhianaji madaraka kwa amani.

Ujumbe wa waangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC umewataka wananchi wa Kenya kuendelea kudumisha amani huku nchi hiyo ya Afrika Mashariki ikisubiri kukamilika mchakato wa uchaguzi.

Tags